Kampuni ya Uber ambayo hutoa huduma ya usafiri ya taxi kwa njia ya mtandao imesitisha huduma zake nchini Tanzania.
Taarifa iliyotumwa na timu ya Uber kwa wateja wa usafiri huo maarufu nchini imesema kuwa wameamua kusitisha huduma zake kuanzia 14 Aprili 2022.
Taarifa hiyo ambayo imetumwa kwenye email za wateja imesema kuwa huduma za UberX, UberXL na UberX Saver hazitapatikana nchini Tanzania.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa sababu ya kusitisha huduma hiyo ni kutokana na kanuni za usimamizi wa sekta hiyo kujenga mazingira ambayo siyo rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara hiyo.
“Tumechukua uamuzi mgumu wa kusitisha kwa muda huduma za UberX, UberXL na UberX Saver nchini Tanzania, bidhaa hizi hazitapatikana kuanzia Alhamis 14 Aprili 2022. Kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hii zimejenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yetu, hadi pale muafaka utakapopatikana.
Huu ni wakati mgumu kwetu sote, lakini hii haina maana kwamba ndio mwisho wa kila kitu.
“Tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija na kujenga mazingira wezeshi na tutarudi na kuendelea na kukupa usafiri wa kutegemewa na wa uhakika ambao umekuwa ukiutumia, baada ya kujiridhisha kwamba mazingira ya kibiashara ni rafiki”.
Discussion about this post