Home BIASHARAUWEKEZAJI 80% ya utalii Tanzania unategemea wanyamapori

80% ya utalii Tanzania unategemea wanyamapori

0 comment 100 views

Takribani asilimia 80 ya utalii wa Tanzania unategemea wanyamapori.

Kutokana na umuhimu huo wa wanyamapori, Tanzania imetenga takribani 32.5% ya eneo lake kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori.

Utalii umekuwa ukichangia 17.2% ya pato la taifa, asilimia 10 katika ajira na 25% ya fedha za kigeni.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki, ameeleza hayo Mei 22, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya mabomu baridi 4000 ya kufukuza tembo kwenye maeneo ya wananchi yaliyotengenezwa na Shirika la Mzinga mjini Morogoro.

Katika hafla hiyo Waziri Kairuki amebainisha kuwa takribani Halmashauri 44 zimebainika kuathiriwa zaidi na changamoto ya wanyamapori.

Mara baada ya kupokea mabomu hayo Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza operesheni maalum katika Halmashauri 20 nchini na inaongozwa na Naibu Katibu Mkuu CP Benedict Wakulyamba.

Wakati Wizara ikipokea mabomu hayo, Bunge la Tanzania kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara hiyo kwa ubunifu wa kuvumbua bomu hilo baridi lililoboreshwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Timotheo Mnzava amesema “naomba kutoa pongezi za dhati kwa Wizara na Shirika kwa kuja na suluhisho hili na natoa wito kwa halmashauri zinazosumbuliwa na Tembo kununua na kutumia mabomu haya ili kupambana na wanyama hao.”

Ameitaka Wizara kuendelea kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji na vijana kwa kuwa Serikali peke yake haitaweza.

“Hii ni kazi ya sisi sote, Serikali peke yake haitaweza ni lazima kuendelea kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa elimu,” ameongeza.

Pia ameiomba Wizara kuendelea kufanya tafiti ili kubuni mbinu nzuri zaidi za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia kuwa Tembo wamekuwa wakizoea mbinu na kuendelea kuleta usumbufu.

Mwakilishi wa wabunge kutoka kwenye majimbo yenye changamoto za Tembo walioshiriki hafla hiyo, Salma Kikwete amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara kwa kuendelea kutatua changamoto ya wanyamapori kuingia katika maeneo ya wananchi.

“Leo kila Mbunge amefurahi kwa kuwa hili ni jambo kubwa ambalo litaleta suluhisho na sasa tunakwenda kurudisha salamu kwa wananchi wetu kazi hii nzuri iliyofanywa na wananchi,” amesisitiza huku akitaka elimu iendelee kutolewa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter