Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania na EU kushirikiana sekta ya maliasili na utalii

Tanzania na EU kushirikiana sekta ya maliasili na utalii

0 comments 63 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Umoja wa Ulaya (EU) zimejadiliana kushirikiana katika Sekta ya Maliasili na Utalii hususan katika uhifadhi wa mazingira, uchumi wa bluu, ufugaji nyuki na uzuiaji wa uwindaji haramu wa mazao ya misitu na wanyamapori.

Hayo yamejiri katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau kilichofanyika Juni 4, 2025 katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Dkt. Chana ameomba Umoja wa Ulaya kusaidia uwekezaji wa kiteknolojia na utafiti katika nishati safi ya kupikia, viwanda vya misitu na kusaidia uanzishwaji wa Maabara ya Sanaa ya Misitu katika Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania – TAFORI.

“Mlengo wetu ni katika suala la matumizi ya teknolojia katika uhifadhi kwa sababu theluthi ya eneo la nchi ni maliasili hivyo tunapaswa kuhifadhi si kwa faida ya Bara la Afrika tu bali kwa dunia kwa ujumla” amesisitiza balozi Dkt. Chana.

Aidha, ameiomba EU kusaidia katika utekelezaji wa Programu mpya ya Maendeleo ya ufugaji nyuki inayozingatia uboreshaji wa maisha hasa kwa jamii katika utoaji wa ajira hasa kwa vijana na wanawake, kusaidia uhifadhi wa rasilimali za nyuki na maliasili nyinginezo ,kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki na kuuza hasa kwenye soko la kimataifa na kuanzisha awamu ya pili ya mradi wa BEVAC.

Kuhusiana na Sekta ya Misitu Waziri Chana amehimiza na kuwakaribisha wadau mbalimbali kuwekeza katika Biashara ya Kaboni ili kukuza maisha ya jamii na Uchumi wa Taifa huku tukiboresha uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu.

Kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, balozi Dkt. Chana amefafanua kuwa zaidi ya asilimia 90% ya kaya nchini Tanzania zinategemea mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia jambo linalochangia takriban asilimia 54 ya ukataji miti nchini Tanzania hivyo kwa kuwekeza katika nishati safi, kutaepusha ukataji miti hovyo na utunzaji wa ardhi kwa maendeleo ya Taifa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!