Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), inaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) kutoka Kanda ya Ziwa kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kanzi Data za Wakopaji (Credit Reference System – CRS).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha BoT, Dkt. Ephraim Mwasanguti, aliwataka washiriki kuzingatia kikamilifu mafunzo hayo ili kupata uelewa wa kina wa matumizi ya mfumo husika.
Alieleza kuwa matumizi sahihi ya CRS yatasaidia kupunguza mikopo chechefu, kuboresha afya ya kifedha ya vyama vya SACCOS na hatimaye kupunguza viwango vya riba kwa wanachama.
“Ndugu zangu, iwapo tutazingatia maelekezo ya mafunzo haya, yatawasaidia kuwajua vizuri wateja wenu watarajiwa. Hii itawawezesha kuchakata maombi ya mikopo kwa ufanisi zaidi na kuwabaini wakopaji wasiofaa, hivyo kuchangia katika uthabiti wa sekta ya fedha,” alisema Dkt. Mwasanguti.
Kwa upande wake, Kaimu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndugu Sojephati Kisamalala, aliishukuru Benki Kuu kwa kuratibu mafunzo haya muhimu kwa wadau wa SACCOS katika Kanda ya Ziwa.
Alisisitiza kuwa mafunzo haya yatasaidia kupunguza idadi ya wakopaji wasio na sifa stahiki na kuongeza ufanisi katika utoaji wa mikopo.
Mafunzo haya yanafanyika katika Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania kilichopo jijini Mwanza, kuanzia Mei 12 hadi 16, 2025, yakiwahusisha washiriki zaidi ya 70 kutoka mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara, Mwanza pamoja na Wilaya ya Geita.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za kifedha kwa vyama vya SACCOS na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa sekta ya fedha nchini.