Home FEDHA Hatua muhimu zitakazokuwezesha kuwa imara kiuchumi

Hatua muhimu zitakazokuwezesha kuwa imara kiuchumi

0 comments 68 views

Ili kufanikiwa kiuchumi unahitaji kuwa na nidhamu ya fedha, mipango na juhudi endelevu juu ya fedha zako.

Hatua ya kwanya ni kufanya tathmini hali yako ya kifedha ya sasa

Fuatilia mapato na matumizi yako, hapa unaweza kutumia program kama MintYNAB, au jedwali rahisi (spreadsheet). Nyingine ni kuorodhesha madeni yako kama yapo (mikopo pamoja na mali zako akiba au uwekezaji wako). Pia unaweza kuweka hesabu za mali zako zote ulizonazo pamoja na madeni.

Hatua ya pili ni kutengeneza bajeti yenye mafanikio

Unapotengeneza bajeti yenye mafanikio ni muhimu kuzingatia kanuni ya 50/30/20. Kanuni hii inaainisha kwamba asilimia 50 ya mapato yako ni kwa mahitaji ya msingi ikiwemo kulipa kodi ya pango (kama umepanga nyumba), chakula, pamoja na matumizi muhimu ya nyumbani.

Asilimia 30 nyingine ni kwa ajili ya mahitaji mengine yasiyo ya lazima, kama sherehe na kujiburudisha, huku asilimia 20 iliyobaki unaweza kuiweka akiba. Ingawaje kanuni hii ya 50/30/20 inaweza kutumika, lakini inaweza isilete mafanikio kw watu wote ambao watatumia kanuni hii, hivyo basi unaweza kuibadili kulingana na malengo yako.

Hatua ya tatu ni kuwa na akiba/hazina ya dharura

Hapa unaweza kuwa na akiba ya miezi mitatu hadi sita ambayo unaweza kuwa umeiweka katika akaunti ya akiba yenye faida kubwa kwa matumizi ya baadae.

Hatua ya nne ni kulipa deni lenye riba kubwa (kama una madeni)

Kama una madeni labda benki au kwenye taasisi nyingine za fedha, anza kulipa deni lenye riba kubwa ili kupunguza gharama kwani kadri deni linavyokaa kwa muda mrefu, riba nayo huongezeka mara dufu. Pia epuka kuchukua mkopo mpya pasipo ulazima wa kufanya hivyo.

Hatua ya tano ni kuongeza mapato yako

Katika kuongeza mapato, hapa unaweza kuomba nyongeza ya mashahara mahali pako pa kazi au kupandishwa cheo na marupurupu mengine kazini. Pia unaweza kutafuta kazi ya ziada ambayo itakuingizia kipato nje na ajira yako, unaweza kuwa mjasiriamali au dereva wa mtandaoni (uber) baada ya muda wako wa kazi, hii itakusaidia kupata kipato cha ziada. Kwa mfano unamiliki gari na unalitumia kwenda kazini, unaweza kujisajili kwenye program za udereva mtandaoni na ukapata abiria wa njia unayoitumia kwenda kazini na kurudi hivyo kujipatia kipato katika mizunguko yako ya kawaida.

Hatua ya sita inalenga katika kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadae

Unatakiwa kuweka akiba kwa ajili ya kustaafu. Kwa waajiriwa hapa hutumika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama NSSF, PSSF na mingine, ambapo asilimia kumi ya mshahara huwekwa katika mfuko husika wa hifadhi ya jamii pamoja na asilimia 10 nyongeza kutoka kwa mwajiri.

Pia unaweza kufanya uwekezaji sio lazima uanze na uwekezaji mkubwa, unaweza kuanza na mtaji mdogo.

Malengo mengine unaweza kufungua akaunti za akiba kwa ajili ya mambo mbalimbali kama elimu, biashara n.k.

Hatua ya saba ni kuishi chini ya kipato chako

Kuishi chini ni kipato chako ni jambo ambalo litakufanya kuweza kupangilia vizuri mapato na matumizi ya fedha zako. Watu wengi hujikuta katika madeni na kufilisika kwa kuishi juu ya kipato chao. Usiwe na matumizi ya juu kuliko kiasi cha fedha unachoingiza. Mfano unakipato cha laki nne kwa mwezi lakini matumizi yako kwa mwezi ni Zaidi ya laki nne, epuka hiyo kwani itakupelekea kuangukia katika madini makubwa usiyoweza kuyalipa.

Pia epuka matumizi yasiyo ya lazima mfano kununua nguo mpya kila wakati na matumizi mengine ya ziada ambayo siyo ya lazima.

 Hatua ya nane ni kulinda uchumi wako

Hapa unaweza kulinda au kuwa na uhakika wa kifedha kwa kuwa na bima ya afya pamoja na wale wote wanaokutegemea. Hii itakusaidia kulinda kipato chako indapo kutatokea tatizo la kiafya kwani bima itakusaidia katika kupunguza gharama za matibabu. Pia unaweza kuwa na bima ya majanga endapo mazingira ya kazi yako ni hatarishi ambayo yanaweza kusababisha ajali wakati wa kazi. Katika hatua hii muhimu, ni vema pia kuandika wosia wa mali unazomiliki.

Katika hatua hizi, hatua ya tisa inaangazia kujifunza na kujiendeleza kielimu mara kwa mara

Hapa ni kwa kusoma vitabu, hususani vinavyohusu maswala ya fedha na uzalishaji, kufuatilia wataalamu wa fedha na watu waliofanikiwa kifedha pamoja kujua fursa zilizopo na zenye mafanikio katika biashara na uwekezaji.

Hatua ya kumi, ni kupitia na kufanya marekebisho ya bajeti yako mara kwa mara

Hapa huenda kuna mabadiliko katika mapato na matumizi yako ya kila siku. Ni muhimu kuipitia bajeti uliyojiwekea ili kufanya marekebisho kama yanahitajika. Pia angalia mwenendo wa uwekezaji wako kila mwaka na kujiwekea malengo mapya kiuchumi.

Kwa kufuata hatua hizi utajenga msingi imara wa kifedha na kufikia mafanikio yako.

Mafanikio ya kifedha yanahitaji mipango, nidhamu ya fedha na mazoea. Anza kwa kujua hali yako kiuchumi, mapato na matumizi, akiba, madeni na kadhalika. Endelea kujifunza, tambua kuwa kila hatua ndogo inaweza kuleta mabadiliko makubwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!