Home FEDHAMIKOPO Mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wakopaji wazinduliwa

Mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wakopaji wazinduliwa

0 comments 69 views

Katika juhudi za kulinda watumiaji wa huduma za fedha dhidi ya manyanyaso ya kifedha na kuhakikisha haki na usawa katika sekta ya fedha, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezindua mfumo mpya wa kushughulikia malalamiko ya wateja uitwao SEMA NA BOT pamoja na Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha.

Halfa ya uzinduzi huo imefanyika June, 05, 2025 jijini Dodoma.

Katika uzinduzi huo, Dkt. Nchemba amesema mfumo wa SEMA NA BOT utakuwa suluhisho kwa changamoto nyingi zinazowakumba wananchi, hususan wale waliokuwa wakinyanyaswa na taasisi zisizo rasmi za mikopo maarufu kama mikopo umiza au kausha damu.

Amesema mikopo hiyo imekuwa chanzo cha mateso kwa wananchi wanaotafuta mikopo ya haraka huku wakikwepa taasisi rasmi za kifedha.

“Kuzinduliwa kwa mfumo wa SEMA NA BOT kutaongeza imani ya umma katika kutumia huduma rasmi za fedha na kuboresha uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha wanaosimamiwa na Benki Kuu,” alisema.

Dkt. Nchemba ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuandaa mfumo unaojibu moja kwa moja changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi, na kuutaja kama utekelezaji wa dhahiri wa falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R kwa kuleta mageuzi katika huduma za fedha.

Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema mfumo wa SEMA NA BOT ni wa kidigitali na utamwezesha mtumiaji wa huduma za fedha kuwasilisha malalamiko kwa njia ya tovuti, simu janja kupitia programu tumishi (Apps), na hata kwa simu za kawaida kupitia USSD.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

“Mfumo huu ni rafiki na utamuwezesha kila mtumiaji wa huduma za fedha kuufikia na kuutumia wakati wowote, bila kujali mahali au uelewa wa teknolojia”, alisema.
Aidha, Gavana Tutuba amesema kuwa mfumo huo utawezesha taasisi za fedha kubaini na kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka, pamoja na kukusanya takwimu za malalamiko yaliyowasilishwa na kushughulikiwa.

Takwimu hizo zitatumika kama nyenzo muhimu kwa taasisi za fedha katika kuboresha huduma zao na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!