Home FEDHAMIKOPO Wachimbaji wadogo washauriwa kukopa mitaji

Wachimbaji wadogo washauriwa kukopa mitaji

0 comment 35 views

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wachimbaji wadogo wa madini kukopa mitaji benki kwani wanao uhakika wa kudhaminiwa na Benki kuu. Majaliwa amesema hayo wakati akifunga maonyesho ya dhahabu, teknolojia ya madini na uwekezaji mkoani Geita.

“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la kawaida sana. Nenda mkakope ili mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu na madini mengine”. Amesema Waziri Majaliwa.

Mbali na hayo, Majaliwa amewaeleza wananchi wa Geita kuwa, siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kujiunga kwenye vikundi ili wawe na malighafi ya kutosha kwa ajili ya mitambo ya kuchenjua dhahabu pamoja na madini mengine.

“Wakuu wa wilaya za mkoa huu simamieni zoezi hili kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa vikundi na mwende mkawasemee benki pale wanapokwama”. Amesisitiza Majaliwa.
Kuhusu makusanyo ya fedha kutokana na mauzo ya dhahabu katika mkoa huo, Waziri Mkuu amesema tangu Aprili mwaka huu, mapato yameongezeka kutoka Sh. 400 milioni hadi Sh. 850 milioni kufikia mwezi Agosti.

Akimkaribisha Waziri Mkuu kutoa neno kwa wananchi waliohudhuria maonyesho hayo, Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema japokuwa sekta ya madini iliongoza kwa kuingizia taifa pato la kigeni kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kutokana na kuuza bidhaa nje ya nchi, sekta hiyo ilichangia pato la taifa kwa asilimia 4.8 pekee. Kairuki amewahakikishia wakazi wa Geita kuwa, lengo la serikali ni kuiwezesha sekta hiyo kuchangia asilimia kumi katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter