Home FEDHA Serikali ya Tanzania kutumia Sh 133.310bn kwa wajasiriamali

Serikali ya Tanzania kutumia Sh 133.310bn kwa wajasiriamali

0 comment 70 views

Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 133.310 kwenye sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kuwawezesha mitaji, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, matumizi ya huduma za fedha, tafiti kuhusu sekta ya fedha na kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye sekta ya fedha.

Hayo yameelezwa jijini Mbeya na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akifungua Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi” kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, yanayofanyika katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.

Amesema Serikali imepanga kutekeleza hayo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/22 -2025/26 ambapo wahusika wakuu ni Taasisi za Fedha na watoa huduma za Fedha.

”Watoa huduma za Fedha watekeleze majukumu yao kulingana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/22-2025/26, Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2021/22-2029/2030 na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (5) wa Elimu ya Fedha (2019/20-2025/26) kwa Maendeleo ya Sekta ya Fedha na Nchi kwa ujumla” ameagiza Prof. Mkenda.

Amesema Serikali imekuwa ikiboresha Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Fedha kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.

Prof. Mkenda amesema katika jitihada hizo Serikali imefanikiwa kuongeza mchango wa Sekta ya Fedha katika ukuaji wa uchumi pamoja na kuongeza upatikanaji na utumiaji wa huduma jumuishi za fedha kutoka asilimia 65 mwaka 2019 hadi asilimia 76 mwaka 2023.

Aidha, ametaja mafanikio mengine kuwa ni watoa huduma Ndogo za Fedha kutambuliwa, kusajiliwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuongezeka kwa upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha wananchi kutumia huduma rasmi za fedha, ambapo jumla ya Mikoa 12 na Halmashauri 65 na wananchi zaidi ya 32,000 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Mei, 2024 hadi Septemba, 2024 walifikiwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter