Jumla ya Shilingi bilioni 1.62 zimekusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Fedha hizo zimepatikana usiku wa Aprili 5, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharamia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Singida. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kuchangisha fedha hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yana lengo la kuhamasisha utoaji wa haki za wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi kwa ujumla ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya Sh milioni 832.8.
Amesema dhumuni jingine la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi michango ya wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na uchumi, Mei Mosi ni fursa ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi duniani kote.
Waziri Mkuu amesema mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, rais wa TUCTA, Tumaini Nyamuhokya, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata.