Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIBIASHARA Maagizo ya Rais Dkt. Samia TRA

Maagizo ya Rais Dkt. Samia TRA

0 comments 212 views

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamisha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda kusimamia usawa katika kulipa kodi.

Rais Dkt. Samia ametoa tamko hilo Januari 23, 2025 wakati wa hafla ya utoaji tuzo za shukrani kwa Mlipakodi Bora wa mwaka 2023/24 zilizotolewa na TRA katika ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.

Aidha, Rais Dkt. Samia amemtaka Kamishna huyo kuchukua hatua za haraka kwa watumishi wanaotengeneza mazingira ya kutokuwa na usawa katika ulipaji wa kodi na yanayochochea rushwa.

“Nakuelekeza kuchunguza mienendo ya watumishi na kuchukua hatua za haraka na bila upendeleo kwa mtumushi yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa ikiwemo kusaidia ukwepaji kodi,” amesema Rais Dkt. Samia.

Ameeleza kuwa, ukwepaji kodi unaathiri wananchi, wafanyabiashara na nchi kwa ujumla, kusababisha kuchelewesha maendeleo ya nchi na kuifanya Serikali kushindwa kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya watu kufanya kazi, biashara na uchumi kuendelea kukua ili Serikali ipate kodi kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za jamii na ustawi wa watu.

“Mwaka 2024, niliunda Tume ya Maboresho ya Kodi nchini ili ifanye thathimini ya mfumo wa kodi na kuleta mapendekezo namna ya kuboresha mfumo wa kodi nchini.

Lengo la Tume hiyo ni kujenga mfumo wa kodi unaoimarisha usawa katika kulipa kodi, unaotabirika, ulio rahisi na usio na usumbufu wenye viwango vya kodi Rafiki,” amesema Rais Dkt. Samia.

Pia ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kuwa na mfumo wa kodi unaorahisisha na kuchunguza shughuli za kiuchumi ili kodi ikusanywe kwa wingi na kuleta maendeleo kwa haraka Zaidi na kupunguza utegemezi wa kibajeti.

Kuhusu matumizi ya TEHAMA, Rais Dkt. Samia ameitaka TRA kutumia mifumo hiyo katika kumhudumia kwa wakati mlipa kodi wa mwisho na kuongeza mapato ya kikodi yanayoendana na uwekezaji uliofanywa katika kujenga uchumi wa kidijitali na kuwarahisishia walipa kodi kutimiza wajibu wao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!