Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania imejipanga kukabiliana na mabadiliko ya sera za nje za Marekani kuhusu misaada kwa nchi za Afrika kwa kutumia rasilimali zake ndani kupitia Bajeti Kuu ya Serikali.
Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Adriano Ubisse, kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Dkt. Nchemba alikuwa akijibu swali la Ubisse, aliyetaka kufahamu mipango ya Serikali ya kukabiliana na uamuzi wa Marekani wa kusitisha misaada yake kwa Bara la Afrika ikiwemo sekta ya afya pamoja na kuweka ushuru wa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka mataifa hayo na mengine duniani kote.
Alisema kuwa Serikali imetenga fedha na kuongeza mafungu ya matumizi kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, kwa ajili ya kugharamia sekta mbalimbali zinazoathiriwa moja kwa moja na uamuzi huo wa Marekani, ikiwemo sekta ya afya.
Dkt. Nchemba alifafanua kuwa Serikali imejipanga kubana matumizi yake ya kawaida na kuelekeza fedha nyingi katika maeneo ya huduma za jamii na sekta za uzalishaji ili kulinda uchumi wa nchi unaokua kwa kasi lakini pia kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii.
“Nchi zetu za Afrika, Tanzania ikiwemo, hatuwezi kuruhusu dira yetu ya maendeleo ikakwazwa na mabadiliko ya kisera ya mataifa mengine, tutachukua hatua Madhubuti za kutenga fedha kwa ajili ya huduma za jamii, kukuza uzalishaji pamoja na ujenzi wa miundombinu ambapo tutapitia upya eneo la matumizi na mapato ya serikali” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo alisema kuwa Serikali imekamilisha Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo imeweka misingi ya kukuza uwezo wa nchi kujitegemea kwa kuimarisha sekta muhimu za uzalishaji, ikiwemo kilimo, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, hatua itakayokuza kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo.