Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Jinsi Zanzibar ilivyotekeleza ilani ya CCM kiuchumi, elimu

Jinsi Zanzibar ilivyotekeleza ilani ya CCM kiuchumi, elimu

0 comments 88 views

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imewasilisha jinsi ilivyotekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/2025.

Hii ni katika kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Akiwasilisha utekelezaji wa Ilani hiyo jijini Dodoma, Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla alielezea jinsi Serikali ilivyotekeleza Ilani hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, uchumi, utalii, miundombinu, afya na sekta nyingine.

Ilani hiyo ilieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeongezeka kutoka asilimia 1.3 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2024 huku Pato la Taifa likiongezeka kutoka Shilingi bilioni 4,780 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 6572.6 kw mwaka 2024.

Ilani hiyo imeonesha kuwa pato la ndani liliongezeka kutoka trilioni 0.856 mwaka 2020/21 hadi trilioni 2.104 mwaka 2023/24 ikiwa ni ongezeko la trilioni 1.248 sawa na ongezeko la asilimia 145.7.

Taarifa ya Ilani imebainisha kuwa ukuaji wa uchumi na ongezeko halisi la Pato la Taifa kwa kipindi cha uongozi wa miaka mitano ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi umechangiwa na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ya Serikali na kuimarika kwa sekta ya huduma, kuimarika kwa shughuli za uwekezaji, kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar pamoja na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchi.

Bajeti ya Serikali imeongezeka kutoka trilioni 1.85 kwa mwaka 2020/2022 hadi trilioni 5.18 mwaka 2024/2025 sawa na ukuaji wa asilimia 228.

“Mabati yamesimamishwa, mabati yameshushwa na mkasi unafanya kazi yake, kinachoonekana ni neema tupu, inayoakisi kesho yenye tumaini na shauku ya kila Mzanzibari wa leo na kesho.

Afya ni neema, na mtu mwenye afya njema huwa na nguvu ya kujitafutia riziki ya halali na kutimiza wajibu wa kiroho.”

Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi nahodha Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeendelea kuhakikisha inatoa huduma za afya bila malipo kuanzia ngazi ya msingi hadi rufaa huku huduma za afya zikiimarishwa kwa kipindi kifupi.

Kwa bajeti ya Shilingi bilioni 104.44 Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi imekamilisha ujenzi wa Hospitali kumi za Wilaya na moja ya Mkoa zenye vifaa tiba vya kisasa Unguja na Pemba.

Hospitali hizo ni pamoja na Kivunge, Pangatupu, Kitogani, Mwera Pongwe, Itimai, Puzini na Chumbuni kwa upande wa Unguja.

Makala hayo yameeleza kuwa kwa upande wa Pemba ni hospitali za Vitongoji, Micheweni na Kinyusini ambazo zote zimekamilika na kufunguliwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi na kupelekea kuimarika kwa huduma za afya.

Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa ya Lumumba ujenzi wake umegharimu Shilingi bilioni 29.984 ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa Zaidi ya laki nane, tisini na tatu elfu, mia moja sitini na tisa wanaoishi Mjini Magharibi na maeneo ya jirani.

Makala ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nane inaeleza kuwa hospitali hiyo pia ina uwezo wa kulaza wagonjwa 208 kwa wakati mmoja.

“Ujenzi wa hospitali mpya umerahisisha na kuondoa adha ya msongamano, sambamba na uimarishwaji wa mifumo ya TEHAMA, ambayo imeunganishwa katika Hospitali zote kwa njia ya mtandao ili kurahisisha taarifa za mgonjwa kupatikana kwa urahisi kutoka Hospitali moja hadi nyingine ili kusaidia kujua historia ya mgonjwa.

Kwa upande wa miundombinu, Serikali imeamua kuajiri watumishi wa kada ya afya kutoka watumishi 559 mwaka 2020 na kufikia watumishi 2008 mwaka 2024.

Mbali na hivyo, Serikali imeweza kusomesha wataalamu 497 katika kada mbalimbali na madaktari bingwa Zaidi ya 19 wamehitimu.

Huduma za Bima ya Afya hazikuachwa nyuma, zikanzishwa mwaka 2023 huku bajeti ya dawa ikiongezeka kutoka bilioni 17 mwaka 2020/2021 hadi kufikia bilioni 40 mwaka 2024/2025 ambapo kwa sasa vituo vya afya vinapata huduma ya dawa kila mwezi badala ya baada ya miezi mitatu ilivyokuwa hapo awali.

“Upatikanaji wa dawa umeimarika kwa Hospitali za ngazi za Wilaya na Mkoa kutoka asilimia 57 mwak 2021 hadi kufikia asilimia 95. Serikali pia imefanikiwa kuokoa fedha nyingi baada ya kufunga mitambo miwili mikubwa ya hewa tiba katika Hospitali za Wilaya Unguja na Pemba.

Kukamilisha ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika Hospitali ya Abdalah Mzee Pemba huku ikiendelea na hatua za mwisho za ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika Hospitali ya Mwera Pongwe, Kitogani na Pangatupu kwa Unguja na Pemba katika Hospitali ya Kinyasini na Kitongoji ambao umegharimu Shilingi bilioni 20.402.

Ilani hiyo inaeleza kuwa Serikali kwa sasa inajivunia ukuaji wa sekta ya afya kutokana na uimarishaji wa huduma za uchunguzi kwa kuongeza vifaa vya uchunguzi katika Hospitali mpya na kongwe.

Vifaa hivyo ni kama CT-Scan, MRI, Xray na Ultra sound na kupelekea kuanzishwa kwa huduma za kibingwa zikiwemo huduma za upasuaji wa nyonga, magoti bandia, usafishaji figo (Dialysis) zimeanzishwa katika Hospitali ya Lumumba Unguja na Abdalah Mzee Pemba.

Huduma za wagonjwa mahututi (ICU) zimeimarishwa kwa Hospitali 113 ikiwemo jengo jipya katika Hospitali ya Abdalah Mzee Pemba pamoja na kukamilisha maabara ya kujifunzia katika Hospitali ya Lumumba ambayo imegharimu Shilingi bilioni 1.252.

Kwa sasa huduma za afya Zanzibar zinapatikana kwa umbali usiozidi kilomita 5 ambapo kila Mzanzibari anapata fursa ya huduma za afya zenye uhakika.

Elimu ni miongozni mwa sekta zilizopewa kipaumbele na Rais Dkt. Mwinyi ambapo kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake bajeti ya elimu imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 265.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia Bilioni 830 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 212.6.

Ongezeko hilo limewezesha bajeti ya maendeleo ya elimu nayo kuongezwa kutoka bilioni 19.4 mwaka 2020/2021 hadi kufikia bilioni 518 mwaka 2024/25.

Kwa upande wa miundombinu imeboreshwa kwa ujenzi wa skuli 149 za maandalizi, msingi na sekondari zenye madarasa 4810 zikiwemo skuli 60 za ghorofa zikihusisha miundombinu ya kisasa ikiwemo maabara za kisasa, maktaba, vyoo vya kisasa vinavyoendana na mazingira ya wanafunzi, kompyuta za kusomea sambamba na ofisi za waalimu.

Watoto wenye uhitaji maalumu ambapo wamewekewa mazingira mazuri ya wao kujifunzia kwa kujengewa skuli maalumu. Skuli hizo ni pamoja na Jendele Unguja na Pojini Pemba kwa bajeti ya Shilingi bilioni 8.7.

Pamoja na hayo vitendea kazi na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi vikanunuliwa ikiwa ni Kompyuta mpakato (laptop) 500, kompyuta 1500, projekta 500 na vishikwambi 6193.

Serikali imewazawadia kompyuta mpakato wanafunzi 4750 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne na sita.

Kwa upande wa ajira Rais Dkt. Mwinyi ametoa ajira mpya za walimu 3531 huku bajeti ya elimu ya juu ikiongezeka kutoka bilioni 11.5 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 33.4 mwaka 2024/2025 ambapo imesaidia wanafunzi wanaopatiwa mikopo ya elimu ya juu kuongezeka kutoka 4,045 hadi 11,495 ikiwa imevuka shabaha ya ilani kwa asilimia 164.

Rais Dkt. Mwinyi, amefanikisha ununuzi wa seti ya viti na meza 115000 pamoja na ujenzi wa dakhalia zaidi ya 19 katika kipindi kifupi jambo ambalo halikuwahi kutokea katika historia ya Zanzibar.

Kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa skuli za msingi kimeongezeka kutoka asilimia 83.9 mwaka 2019 hadi asilimia 103.8 mwaka 2025.

Kiwango cha ufauli wa wanafunzi wa kidato cha pili umeongezeka kutoka asilimia 76.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 84.4 mwaka 2024.

Kwa upande wa kidato cha nne, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 66.3 mwaka 2021 hadi asilimia 82 mwaka 2024, huku kidato cha sita ukiongezeka kutoka 98.8% hadi 99.9% kwa kipindi hicho.

Hii inaonesha kuwa mchango wa Rais Dkt Mwinyi katika sekta ya elimu ni mkubwa kwani amefanikisha kuvuka lengo la ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yam waka 2020/2025 kwa asilimia 184 mpaka sasa.

Serikali imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kupunguza gharama za uunganishaji wa huduma za umeme kutoka Shilingi 464,000 hadi Shilingi 200,000 kwa wateja wasiozidi urefu wa mita 30 na kutoka Tsh 1,700,000 kwa wateja wa nguzo moja na kufikia Tsh. 200,000.

Hii imerahisisha wananchi wengi kuunganishiwa huduma ya umeme ambapo changamoto iliyokuwa inawasumbua wananchi na wawekezaji juu ya upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme imepata ufumbuzi.

Rais Dkt. Mwinyi amefanikisha ujenzi wa vituo vya kuongeza nguvu ya umeme katika maeneo ya Kaskazini na Kusini Unguja na Pemba.

Kwa upande wa miundombinu, serikali imefanikisha kuiunganisha na kuileta pamoja Zanzibar kwa kujenga barabara kwa zaidi ya kilomita 500, huku akifanikisha ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 100.9 ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji.

Kuimarika kwa mtandao wa barabara ni mafanikio makubwa kuwahi kutokea Zanzibar na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wa sekta ya anga, Serikali ya awamu ya nane imefanya maboresho katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sheikh Aman Abeid Karume kwa kuongezewa jengo la abiria la Terminal II na kujengwa upya jengo la abiria Terminal I VIP ambapo ujenzi wake umefikia 84% pamoja na ujenzi wa eneo maalum la biashara.

Idadi ya abiria wa kimataifa wanaotumia uwanja huo imeongezeka kutoka abiria 840559 mwaka 2020 hadi kufikia 2140956 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 254.7 na kufanya mapato ya Serikali yatokanayo na uwanja huo kuongezeka kutoka  bilioni 11.641 hadi bilioni 40.209 sawa na ongezeko la 254.4% kwa kipindi hicho.

Kwa kipindi cha uongozi wake,Rais Dkt. Mwinyi amefanikisha ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, uimarishaji wa Bandari ya Mkokotoni, Mkoani na ujenzi wa Bandari ya Shumba mjini na Wete, uimarishaji wa Bndari Wesha na Malindi.

Pia Rais Dkt. Mwinyi amefanikisha ujenzi wa masoko mbalimbali ili kuwainua wananchi kiuchumi pamoja na ujenzi wa vituo vya daladala.

Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi imetoa Shilingi Bilioni 60 ambapo kati ya hizo Bilioni 29 zimeelekezwa kwenye uchumi wa buluu, milioni 16 ujenzi wa masoko na bilioni 15 zimetolewa kuwezesha wananchi kiuchumi.

Mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Shilingi bilioni 35 imetolewa kwa wananchi kupitia program mbalimbali kwa wanufaika Zaidi ya elfu ishirini na nne na kuzalisha ajira mpya elfu sabini na tano.

Sekta ya uwekezaji ni miongoni mwa sekta zilizofanikiwa katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Dkt. Mwinyi. Serikali kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibra (ZIPA) imefanikiwa kusajili jumla ya miradi 466 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.08 na kutoa ajira rasmi zisizopungua 24711 na zisizo rasmi Zaidi ya 100,000.

Kuongezeka kwa miradi kunatokana na maboresho ya Sheria ya Uwekezaji ambayo imeondoa changamoto kwa wawekezaji na kuweka mazingira wezeshi bila bughudha yoyote.

Maboresho hayo yanatokana na uwepo wa Sheria mpya ya Uwekezaji Namba 10 ya Mwaka 2023 ambayo inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani kwa kupata punguzo la mtaji wa kuwekeza ambapo kwa sasa mzawa anaweza kuwekeza kwa mtaji wa Dola za Marekani laki moja huku Diaspora anawekeza kwa mtaji wa Dola laki mbili.

Utalii ndio sekta mama kwa uchumi wa Zanzibar ambapo inachangia Pato la Taifa kwa asilimia 30 na imetoa ajira rasmi 33000 na zisizo rasmi 66000 na kuchangia pesa za kigeni kwa 80%.

Katika uongozi wake Dkt. Mwinyi yameshuhudiwa mafanikio makubwa katika sekta ya utalii ambapo watalii wameongezeka kutoka watalii laki tatu tisini na nne elfu, mia moja themanini na tano mwaka 2021 hadi kufikia watalii laki saba, elfu thelathini na sita mia saba hamsini na tano mwaka 2024 sawa na ongezeko la 89.9%.

“Watalii 2,842,889 wametembelea Zanzibar kwa kipindi cha 2020 hadi Aprili 2025,” imeeleza Ilani hiyo ya CCM.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!