Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Kwanini unaendelea kuwa maskini japokuwa umeajiriwa?

Kwanini unaendelea kuwa maskini japokuwa umeajiriwa?

0 comment 29 views

Watu wengi bado wamekuwa na hali ya chini kiuchumi licha ya kwamba wanafanya shughuli mbalimbali ambazo zinawaingizia kipato. Wote tunaweza kukubaliana kwamba fedha ni muhimu sana katika maisha na ndio funguo katika milango yote ya maendeleo. Huwezi hata kupata maji masafi pasipo kutumia fedha. Hivyo basi ni muhimu kujiuliza, kwanini wengi hawana maendeleo licha ya kuwa wanaingiza kipato kila baada ya mwezi au muda uliopangwa?

 

Mojawapo ya sababu zinazopelekea hali hii ni watu wengi kuwa na chanzo ama njia moja tu ya kutengeneza fedha. Anakuwa tegemezi kwa namna hiyo moja tu ili kupata fedha. Hili sio jambo baya lakini umefikiria itakuaje kama ghafla ukaondolewa kazini? Unafanyaje kama ukipata tatizo kipindi ambacho unasubiria fedha zako? Mazoea ya kuwa na chanzo kimoja cha fedha hayampi nafasi mtu kujiimarisha kiuchumi na ndiyo maana wengi huendelea kubaki katika hatua moja kimaisha.

 

Changamoto nyingine inayopelekea wengi kuwa maskini japokuwa wanafanya shughuli za kiuchumi ni uelewa mdogo katika masuala ya uwekezaji. Watu wengi bado hawaelewi faida za kuwekeza. Hali hiyo inapelekea wao kutumia fedha zao katika matumizi mengine ambayo hayafungui milango kifedha. Ni muhimu kuanza kuwekeza katika shughuli ndogondogo ili kujenga daraja lingine linaloweza kukuingizia kipato ambacho kitasaidia kufanikisha shughuli nyingine za maendeleo.

 

Gharama za maisha nazo zinazidi kupanda juu. Hali hivi sasa hapa nchini inamlazimu mtu kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika mahitaji mbalimbali ya kila siku. Hakuna anayeweza kufanya kazi vizuri bila kuwa na afya njema. Afya njema inahitaji lishe bora na hizi zote ni gharama ambazo haziwezi kuepukika. Kuna gharama nyingine kama ada za shule pamoja na kodi za nyumba ambazo kwa kawaida zinakuwa juu hivyo huchukua asilimia kubwa ya kipato cha mtu. Kutumia kiasi kikubwa cha fedha kunapelekea mtu kubakia na akiba ndogo tu, fedha ambayo anashindwa kufanyia mambo mengine ya msingi ili kujiendeleza kiuchumi.

 

Ili kukua kiuchumi na kuweza kujiletea maendeleo ni vizuri kupanga bajeti yako vizuri hata kama unachoingiza ni kidogo tu. Ni muhimu kuwa na akiba ambayo itakusaidia baadae. Pia tujenge mazoea ya kuwekeza hicho kidogo tulichonacho. Ni wakati wa kuachana na dhana ya kwamba matajiri pekee ndio wawekezaji. Ni vizuri kufanyia kazi malengo yako bila kukata tamaa mpaka ufikie pale ambapo unataka. Jiwekee malengo na amua kuwa unataka kubadilisha maisha yako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter