Tanzania imepiga marufuku uingizwaji wa mazao yoyote ya kilimo kutoka Afrika ya Kusini na Malawi kuingia nchini Tanzania.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ametoa tamko hilo la serikali ya Tanzania Aprili 23, 2024.
“Kama waziri wa Kilimo sijapokea notisi yoyote, mazungumzo yanaendelea na yanaongozwa na Waziri wetu wa Mambo ya Nje, lakini wakati mazungumzo yanaendelea sisi hatuwezi kuendelea kuishi kuwa (denie right) kunyimwa haki hiyo.
Natangaza rasmi kuanzia usiku huu mambo yafuatayo kwa nchi hizi mbili, Afrika ya Kusini imekuwa ikiingiza Tanzania fresh apples, kuanzia leo ni marufuku kuingiza fresh apples ya Afrika Kusini Tanzania.
Waziri Bashe ameeleza kuwa mbali na apple, Afrika ya Kusini inaingiza Tanzania matunda mbalimbali ikiwemo zabibu na mengine ambapo nayo amepiga marufuku kuingizwa nchini Tanzania.
“Hatutaruhusu zao lolote linalotoka Afrika Kusini linalohusiana na kilimo ndani ya nchi yetu,” ameeleza Waziri Bashe.
Kwa upande wa Malawi serikali ya Tanzania imesema haitaruhusu zao lolote la kusafirishwa kutoka Malawi kupita nchini Tanzania.
“Mpaka sasa Malawi hawajafuta notisi waliyoitoa, ninatangaza rasmi, ni marufuku mazao yoyote ya kilimo kutoka Malawi kuingia ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia leo.
Mbali na hapo, kwa nchi zote mbili hizi, hasa Malawi hatutaruhusu zao lolote la transit kupita ndani ya Jamhuri ya Tanzania.
La pili kuhusu Malawi, mahindi yote waliyoyanunua kwa ajili ya kutatua tatizo lao la njaa kwao hayatoenda Malawi, hatutayapeleka.
La tatu, tarehe moja mwezi wa tano walikuwa wanaanza kuchukua mbolea kwa ajili ya maandalizi ya msimu wao wa kilimo kutoka Tanzania, hatutaruhusu mbolea yoyote kwenda Malawi,” amesisitiza Waziri Bashe.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda biashara kati ya Tanzania na nchi hizo mbili na wala haihatarishi usalama wa chakula nchini.
“Hakuna Matanzania atakufa kwa kukosa zabibu ya Afrika Kusini, tunachukua hatua hii kulinda biashara yetu, hii ni biashara n ani lazima wote tuheshimiane,,” amesema Waziri Bashe.
Wiki iliyopita, Malawi na Afrika ya Kusini zilizuia shehena ya ndizi kutoka Tanzania kuingia katika nchi hizo jambo lililopelekea Waziri Bashe kutoa siku saba kwa nchi hizo kuruhusu mazao ya Tanzania kuingia katika nchi hizo.