Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amekabidhi Magari 38 yenye thamani ya shilingi Bilioni 4.2 kwa ajili ya kusimamia na kutekekeza majukumu ya Sekta ya Kilimo, pamoja na magari saba ya mitambo ya uchimbaji visima.
Magari hayo yamekabidhiwa Mei 12, 2025, jijini Dodoma ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) magari (14) kwa ajili ya kusimamia na kudhibiti utoroshaji wa mazao mipakani.
Taarifa kutoka Wizara ya Kilimo inaeleza kuwa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limepewa magari matano kusimamia Vyama vya Ushirika na Vyama vya Msingi huko Bodi ya Mkonge Tanzania ikipewa magari mawili kwa ajili ya kuendesha shughuli za Tasnia ya Mkonge, lengo ikiwa ni kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia Agenda 10/30.
Aidha, mitambo saba ya Uchimbaji Visima imekabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa ajili ya uchimbaji wa visima kwa wakulima hususan wakulima wadogo.
Mitambo hiyo ina uwezo wa kuchimba visima hadi mita 300 na mitambo mingine ina uwezo wa kuchimba visima hadi mita 1800.
“Hatua hii inaenda sambamba na lengo la Serikali katika utoaji wa ruzuku kwa wakulima , ambapo ukiachana na ruzuku ya mbegu na mbolea pia imelenga kutoa ruzuku ya uchimbaji wa visima pamoja na huduma za zana za kilimo kwa wakulima,” imesema taarifa hiyo.
Sambamba na hilo Waziri Bashe pia amekabidhi imagari (20) kwa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji kwa ufanisi zaidi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar, Makamu Mwenyeketi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mariam Ditopile, Menejimenti ya Wizara na watumishi wa Wizara, Taasisi/Bodi za Wizara ya Kilimo.