Home KILIMOKILIMO UFUNDI Waziri Mkuu aagiza ufuatiliaji wa watendaji Vyama vya Ushirika

Waziri Mkuu aagiza ufuatiliaji wa watendaji Vyama vya Ushirika

0 comments 173 views

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iimarishe na kufanya ufuatiliaji wa watendaji wa Vyama vya Ushirika ili wazingatie maadili ya utumishi wa ushirika, uwazi, uwajibikaji na utawala bora, na hivyo kuwavutia wanachama na wawekezaji.

Pia Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo, pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, iharakishe na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati yote iliyopitishwa, hususan katika maeneo ya teknolojia ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo, na masoko ya mazao.

Ametoa maagizo hayo Aprili 27, 2025 wakati akizindua mdahalo wa Upatikanaji Mitaji ya Fedha za Maendeleo ya Ushirika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Sambamba na uzinduzi wa ripoti ya Mwaka ya Kilimo kwa mwaka 2022/2023, 2023/2024.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akizindua ripoti ya Mwaka ya Kilimo kwa mwaka 2022/2023, 2023/2024. Kushoto ni Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzisisitiza taasisi za kifedha, zikiwemo benki na mifuko ya maendeleo, kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyama vya ushirika kwa kuweka mifumo rafiki ya upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo.

Amewataka wakulima na wananchi kwa ujumla kujiunga na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa, ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.

“Wadau wote wa maendeleo, endeleeni kushirikiana na Serikali katika kutoa rasilimali, utaalamu na ubunifu unaohitajika katika kuendeleza sekta hii muhimu. Wizara ihakikishe maandiko ya taarifa zilizozinduliwa zinaandaliwa pia kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika nazo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Sekta ya Ushirika nchini inaendelea kuimarika kwa kasi, ikiwa ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa katika maeneo mbalimbali.

“Hadi sasa, Tanzania inajivunia kuwa na zaidi ya vyama 7,000 vya Ushirika vilivyosajiliwa, vyenye jumla ya wanachama zaidi ya milioni nane. Vyama hivi vinajumuisha sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, uvuvi, madini, biashara na huduma za kifedha.”

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua madhubuti za kuleta mageuzi katika Sekta ya Ushirika ikiwemo kuboresha mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa vyama vya ushirika pamoja na kuimarisha masoko ya mazao kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

“Kuwapatia Maafisa Ushirika vitendea kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuboreshwa kwa upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika na kuimarishwa kwa huduma za kifedha kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika (COOP Bank).”

Akizungumzia uzinduzi rasmi wa mradi wa Mashamba Makubwa unaofadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania, Waziri Mkuu amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

Amesema “mradi ambao nimeuzindua leo, utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030. Gharama ya jumla ya utekelezaji wa BBT Project 1 ni Dola za Marekani milioni 241.27, ambapo AFDB itachangia Dola milioni 129.71, sawa na asilimia 53.76 ya gharama hiyo. Serikali ya Tanzania itachangia asilimia 46.24 ya mahitaji hayo ili kukamilisha mradi huu.”

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema ushirika ni njia pekee inayowajengea uimara wanaushirika na kwamba benki ya ushirika inakwenda kurahisisha malipo ya wakulima ambapo amesema benki hiyo inamtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 50 na itakuwa na mawakala zaidi ya 50 nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Ushirika (Coop Bank), Profesa Gervas Machimu amesema benki hiyo itakuwa nguzo ya maendeleo ya ushirika mijini na vijijini, itarudisha heshima ya ushirika na kuchochea uchumi wa wananchi.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Tume ya Vyama vya Ushirika, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya Ushirika itaendeshwa kisasa zaidi na itakuwa na ushindani na kutoa taswira ya ushirika wenye tija.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!