Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza rasmi kutumia ndege nyuki (drones) kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa misitu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kisasa wa kukabiliana na vitendo haramu vinavyoathiri rasilimali za misitu nchini.
Hatua hiyo imezinduliwa Juni 2, 2025, katika viwanja vya Ofisi ya Kanda ya Kusini ya TFS mkoani Mtwara, ambako ndege hizo zilifanyiwa majaribio mbele ya maafisa wa uhifadhi na marubani waliopata mafunzo ya kuziongoza.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Kamanda wa Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa alisema matumizi ya drones ni hatua muhimu ya kimkakati katika kuimarisha ufuatiliaji wa maeneo ya misitu na kuongeza ufanisi wa kazi za doria na ulinzi.
“Teknolojia hii itaongeza uwezo wetu wa kubaini kwa haraka uhalifu wa kimazingira unaoendelea ndani ya misitu, ikiwemo uvunaji haramu wa mbao, uchomaji moto wa misitu, utengenezaji haramu wa mkaa, pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa matumizi ya kilimo au makazi,” alisema Mpokigwa.

Ndege nyuki (drones) zitakazotumika kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa misitu.
Aliongeza kuwa matumizi ya ndege hizo yataongeza tija katika shughuli za uhifadhi kwa kurahisisha doria katika maeneo magumu kufikika, kukusanya taarifa kwa usahihi kupitia kamera za kisasa zenye uwezo wa kuona hata usiku au kwenye maeneo yenye uoto mnene, na kupunguza gharama za ulinzi ikilinganishwa na mbinu za kawaida.
“Mbali na kupunguza gharama za mafuta na nguvu kazi, teknolojia hii pia itasaidia kuwalinda wahifadhi kwa kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa doria za ana kwa ana,” alieleza.
Mpokigwa aliwataka wahifadhi wa ngazi ya wilaya kote nchini kutumia fursa hiyo kwa weledi, ili kuhakikisha usalama na uendelevu wa misitu ya Tanzania unalindwa kwa kutumia maarifa ya kisasa.
“Huu ni wakati wa kutumia teknolojia kama silaha mpya ya kulinda misitu yetu. Wahifadhi wanapaswa kuwa mbele katika matumizi ya drones ili kutambua waharibifu mapema na kuchukua hatua kabla athari hazijatokea,” alisisitiza.