Mtangazaji ambae pia ni mchoraji katuni wa Tanzania Masoud Kipanya amesema tangu mwaka 2013 alikuwa na ndoto za kutengeneza gari.
Kipanya amesema hayo baada ya kuzindua gari lake la kwanza la umeme kutengenezwa nchini Tanzania April 02, 2022.
Kipanya, amesema gari hilo la umeme ni wazo lake binafsi la ubunifu ambalo lilimchukua miezi 11 kukamilika.
Gari hilo linaloitwa Kaypee Motor ni rafiki kwa mazingira kwa sababu halitumii nishati ya mafuta badala yake linachajiwa kwa saa sita kabla ya kutumika.
“Hili ni gari la nguvu sana ambalo ukinunua unapata na chaji yake,” alisema Kipanya.
Katika mahojiano na kituo cha habari cha Clouds Kipanya amesema “tangu mwaka 2013 nilikuwa na ndoto ya kutengeneza gari na miaka yote nilikuwa naijenga na kuibomoa na ilifika wakati nikawa nataka kiwanda kiwe Bagamoyo na nikapata sehemu nikajenga na ilivyokamilika nyumba nikagundua hii ni nyumba ya kuishi zaidi hapatoshi.
Nikapata eneo jingine na baada ya kujenga msingi nikagundua panahitaji hela nyingi kwa ajili ya kupatengeneza ikabidi nipaache.
Mwaka 2019 nilikutana na Mr Maganga kutoka Sido na akanipa maelezo nikaandika barua ya kutaka eneo na nikapata eneo kama ningekuwa nimelipata kwa mtu binafsi basi ningekuwa nimelipa hela nyingi sana hivyo nilivyopata eneo baada ya kumaliza kulikarabati Corona ikawa imeingia ikabidi niache kwanza ipite ndiyo nirudi tena kuanza kupambania ndoto yangu”.
Kuhusu kipaji hicho Kipanya amesema “mimi napenda kutengeneza nikiona boti njaa yangu sio kuimiliki bali najiuliza hawa wametengenezaje maana ni binadamu kama sisi na wao wamezaliwa na toka nipo mdogo napenda kutengeneza vitu na hata nikiona nyumba nzuri huwa nawaza imejengwaje na huku ninapoelekea nakwenda kuanzisha kampuni ya Real estate kuanza kuzi- design na kuzijenga mwenyewe”.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Hoteli ya Dar es Salaam Serena na kuhudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara nchini.
Discussion about this post