Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amemtaka mkandarasi kutoka Kampuni ya CHICO anaetekeleza mradi wa ujenzi wa mto Ng’ombe kurudi eneo la kazi na kukamilisha kazi iliyobaki.
RC Makalla ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua miradi na kukuta mkandarasi hayupo eneo la kazi licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 60 ya fedha.
Makalla amesema lengo la mradi huo ni kumaliza kero ya mafuriko kwa wananchi wa eneo hilo.
Aidha RC Makalla amemuelekeza mkandarasi kuongeza nguvu ili kazi iweze kukamilika na kukabidhiwa kabla ya November mwaka huu.
Kuhusu wananchi waliolipwa fidia ya zaidi ya Sh. Bilioni sita na bado hawajaondoka, RC Makalla ameelekeza wote waliolipwa kupisha mkandarasi akamilishe kazi ambapo amesema atapita kila wiki kukagua maendeleo ya ujenzi.
Hata hivyo RC Makalla amewataka TARURA kumsimamia mkandarasi huyo aanze ujenzi wa barabara ya mtaa huo ikiwa ni baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa miundombinu ya Barabara hiyo.
Mradi wa ujenzi wa mto Ng’ombe una urefu wa km 8.5.
Discussion about this post