Home Uncategorized Walemavu na wenye mahitaji maalum wapatiwe fursa sawa

Walemavu na wenye mahitaji maalum wapatiwe fursa sawa

0 comment 56 views

Hivi karibuni tumeshuhudia serikali ya Tanzania ikionyesha uthubutu wake katika kujenga usawa miongoni mwa wana jamii kwa kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi watu wenye ulemavu na wenye uhitaji maalum ikiwa ni kutambua umuhimu wa watu hao katika jamii. Hii ni hatua kubwa ambayo nchi za Ulaya zimeshapiga  ukilinganisha na nchi zetu ambazo kwa sasa zimeonesha uthubutu.

Serikali kupitia awamu ya nne iliweza pia kutoa msaada wa bajaji kwa walemavu kadhaa maeneo ya Kariakoo ikiwa ni kutambua umuhimu wa kundi hilo katika uzalishaji, hali ambayo imewasaidia kujitegemea na kuendesha maisha yao.

Tumeshuhudia walemavu na watu wenye mahitaji maalum wakipewa nafasi mbalimbali serikalini na sekta binafsi huku nafasi za ubunge pia zikiongezeka kwa  zikiongezwa. Serikali imekuwa ikitambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi binafsi na za serikali katika kutambua umuhimu wa watu walemavu na wenye uhitaji maalumu katika jamii.

Februari mwaka huu, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alihudhuria hafla ya chakula cha mchana pamoja na walemavu na watu wenye uhitaji maalum iliyoandaliwa na Dkt. Reginald Mengi na kusema kuwa serikali iko bega kwa bega kushirikiana na mashirika, taasisi na asasi mbalimbali ambazo zimekuwa zikionyesha mchango wake katika kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu alitoa mchango wa Tsh. Milioni 10 na kutoa ushauri kwa mfanyabiashara huyo kuanzisha taasisi ya Reginald Mengi Disabled Foundation ili kuwasaidia walemavu.

Mbali na serikali zimekuwepo taasisi, mashirika na asasi mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwasaidia walemavu na watu wenye mahitaji maalum kuzifikia ndoto zao ikiwemo elimu na malezi bora. Mfano wa Taasisi hizo ni kama Tanzania Albino Society (TAS) Asasi ya kuendeleza watoto wa tanzania (AKUWATA), CCBRT, African Children Life Vision Recovery Foundation, Haki Elimu, Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) n.k  ambazo zimekuwa zikitetea na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum na walemavu.

Suala la ukosefu wa fursa za kutosha kwa walemavu ni  kubwa sana na limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa walemavu walio wengi kushindwa kuzifikia ndoto zao  za mafanikio kama walivyo watu wengine.

Hii inatokana ukosefu wa miundombinu bora na mazingira rafiki kwa walemavu kuweza kuzichangamkia fursa zinazotolewa. Licha ya  serikali ya awamu ya tano kuonyesha uthubutu katika hili lakini bado jamii ina mchango mkubwa katika kupigania haki za walemavu ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha katika shughuli za uzalishaji.

Nini kifanyike ili kuhakikisha kunakuwepo na mazingira bora na rafiki kwa walemavu na watu wenye uhitaji maalumu kushiriki shughuli za uzalishaji?

  1. Kuondoa dhana potofu juu ya walemavu na watu wenye uhitaji maalum – Dhana ya kudai walemavu hawawezi kupata elimu bado ipo miongoni mwa watanzania, lakini pia dhana ya kuamini mlemavu hawezi kufanya kazi kwa ufanisi sawa na mtu asiye na ulemavu nayo imekuwa changamoto miongon mwa wana jamii wakiamini kuwa mlemavu ni mtu wa kubaki nyumbani tu, hali inayopelekea kucheleweshwa kwa maendeleo ya nchi kwani hata walemavu wanayo nafasi ya kushiriki katika uzalishaji mali.
  2. Kuwaandalia mazingira mazuri ya kazi- Kuna haja kubwa ya walemavu kuandaliwa mazingira mazuri na rafiki katika maeneo yao ya uzalishaji ikiwa ni pamoja na miundombinu bora ya majengo ikiwemo ofisi na vyoo.
  3. Kuondoa kabisa unyanyapaa- Kuwajali walemavu na kuwaonyesha kuwa ni watu muhimu katika kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi kwa kuwapa motisha ya kazi, kutumia lugha rafiki kuwasiliana nao kuwapa kipaumbele katika shughuli zihusuzo ujasiliamali.
  4. Kuwajengea uthubutu na hali ya kujiamini- Watu wenye mahitaji maalum na wale wenye ulemavu wanahitaji kujengewa hali ya kujiamini na kuthubutu kufanya maamuzi ikiwemo kujishughulisha na ujasiliamali.Wahudhurie semina, warsha na makongamano ambayo yatawasaidia kujijengea hali ya kujiamini na kuchukua maamuzi katika kujiletea maendeleo.

Kuna umuhimu gani wa watu wenye ulemavu na uhitaji maalumu kushiriki katika shughuli za uzalishaji?

  1. Itasaidia kupunguza hali ya utegemezi katika jamii. Endapo walemavu nao watapewa fursa na kuonyesha juhudi zao kuzikimbilia fursa zilizo mbele yao ni dhahiri kuwa taifa na jamii kwa ujumla itapunguziwa majukumu ya kulea kundi hili
  2. Itasaidia kuondoa dhana mbovu juu ya watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu- Endapo kundi kubwa la watu wenye ulemavu litashiriki katika uzalishaji jamii itaondokana na Imani mbovu juu ya walemavu kwa kuwa watakuwa na nafasi ya kuonyesha mchango wao katika jamiii.
  3. Watasaidia kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla- Ni dhahiri kuwa wapo watanzania wenye ulemavu ambao wameonyesha uthubutu wao kwa kugundua mbinu mbalimbali za kiuzalishaji, ujasiliamali pamoja na kujihusisha na siasa,hali inayotia hamasa na chachu katika kuleta maendeleo ya taifa letu.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter