Home VIWANDAMIUNDOMBINU Serikali ya Tanzania yaweka nguvu ujenzi miundombinu

Serikali ya Tanzania yaweka nguvu ujenzi miundombinu

0 comments 195 views

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inaweka nguvu katika masuala ya ujenzi wa miundombinu hususani ya Reli ya Kisasa (SGR) ili kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji.

Amesema hayo jijini Warsaw Poland wakati wa mkutano wake na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye pia anasimamia nchi ya Poland,  Hassani Iddi Mwamweta, wakati wa ziara yake ya kikazi nchini humo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa vipande viwili vya Reli ya Kisasa vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma vimekamilika na kuanza kufanya kazi ambapo kipande cha tatu na nne kutoka Makutopora hadi Tabora na Tabora hadi Isaka ndilo eneo ambalo zinatafutwa fedha ili kukamilisha ujenzi wake.

Aidha, Dkt. Nchemba alimpongeza Balozi Mwamweta kwa kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi katika nchi anazoiwakilisha Tanzania na kusisitiza kuwa Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa uwekezaji na kumtaka aendelee kuhimiza uwekezaji ambao utachangia kukuza uchumi wa nchi.

Alisema kuwa miundombinu mingine iliyopewa kipaumbele ni pamoja na nishati, na miundombinu ya uzalishaji ya kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili ambayo ina lengo la kutengeneza kesho iliyobora zaidi na kusisitiza umuhimu wa vijana kupatiwa ujuzi wa kuzalisha pamoja na kutafuta masoko.

Kwa upande wake Balozi Mwamweta, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu yake, alieleza kuwa jitihada zinazofanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Reli zinaonekana na wadau wa maendeleo, jambo ambalo linarahisisha kazi yake ya kuinadi nchi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kuwa nchi nyingi zilizoendelea katika Bara la Ulaya ziliwekeza kwenye miundombinu wezeshi kama Reli na kuweza kuchochea kwa kasi maendeleo yao jambo ambalo Tanzania pia imekuwa na mwelekeo huo ambao matokeo yake yanaonekana kwenye duru za kimataifa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!