Home VIWANDAMIUNDOMBINU Ubia wahitajika kuipunguzia serikali gharama za miradi

Ubia wahitajika kuipunguzia serikali gharama za miradi

0 comment 36 views

Wataalam wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini wameagizwa kuhakikisha miradi yote mikubwa yenye mvuto wa kibiashara nchini inatekelezwa kwa njia ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership) ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi hiyo.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Elmaamry Mwamba wakati akifungua Kikao Cha kuimarisha ushirikiano kati serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara kuhusu masuala ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Alisema utekelezaji wa miradi kupitia PPP ni sehemu ya kujenga uchumi imara na ni suala ambalo linatekelezwa na nchi nyingi ulimwenguni.

“Msiogope, hata nchi zilizoendelea zinateleza miradi yao kupitia PPP, ukiangalia madaraja na majengo mbalimbali wameyatekeleza kupitia PPP, Sekta Binafsi wakipewa nafasi wanafanya vizuri”, alibainisha Omolo.

Aliwaagiza wataalam hao kukuza uelewa wa dhana ya PPP kwa wadau mbalimbali kwa kuwa bado kuna changamoto ya uelewa wa dhana hiyo pamoja na faida zake.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar Rashid Ali Salim, aliwaagiza wataalam hao kuhakikisha wanayafanyia kazi yale yote waliyokubaliana katika kikao hicho hususani suala la kuwa na mkakati wa pamoja wa kuuza fursa na kuibua miradi ya pamoja ya PPP ili kuimarisha sekta ya PPP nchini.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar Rashid Ali Salim.

Naye, Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha, Bashiru Taratibu, alisema katika kikao hicho kuna masuala mbalimbali wameazimia kuyatekeleza ikwemo maboresho ya sheria ili kurahisisha shughuli za PPP nchini hususani katika kutekeleza miradi ya pamoja katika ya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Tumejadili kuhusu miradi ya pamoja ambayo Sekta Binafsi inaweza kutekeleza kama mradi wa Daraja la Dar es Salaam hadi Zanzibar, lakini kila sehemu wana Sheria yao ya PPP, kwa hiyo tumekaa kuona namna bora ya kutekeleza suala hilo iwapo mwekezaji atajitokeza”, aliongeza Taratibu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter