Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imevifikishia huduma ya umeme Vitongoji 284 katika Jimbo la Arumeru Mashariki kati ya Vitongoji 330.
Kapinga ameyasema hayo Juni 03, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dkt. John Danielson Pallangyo aliyeuliza ni lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA katika Vitongoji 37 ambavyo vipo gizani katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji 17 vipo katika hatua ya utekelezaji kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification IIB) na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA), aidha, katika Vitongoji 29 zabuni imetangazwa ili kupata wakandarasi wa kutekeleza miradi kupitia mradi wa kupeleka umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB).
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Arumeru Mashariki kufikiwa na umeme.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dkt.John Danielson Pallangyo aliyeuliza kuhusu Kata za Arumeru Mashariki zinazo pata maji kutoka msitu wa mlima Arumeru na kuwa na flouride ambapo Kampuni ya Kweka imejitolea kuweka mtambo wa kusafisha lakini kinachohitajika ni umeme, Kapinga amesema tayari Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kukipelekea umeme wa uhakika Kitongoji cha Seneto Kata ya Legeruki kwa ajili ya kutibu flouride katika maji.
Akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Alois Ndakidemi aliyeuliza Serikali itakiunganishia lini umeme Kitongoji cha Orera kilichopo Kijiji cha Mweka, Kapinga amesema katika Jimbo la Moshi Vijijini yupo Mkandarasi anayetekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya kila Mbunge na kuongeza kuwa Kitongoji hicho kipo katika orodha hiyo ya mkandarasi.