Home VIWANDAUZALISHAJI Afrika yaaswa kuimarisha ukusanyaji rasilimali za ndani kukabili misaada inayopungua

Afrika yaaswa kuimarisha ukusanyaji rasilimali za ndani kukabili misaada inayopungua

0 comments 96 views

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sauda Msemo, amezitaka serikali za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali za ndani ili kupunguza utegemezi mkubwa kwa misaada ya kigeni inayopungua.

Akizungumza Aprili 28, 2025 katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Uchumi wa Kanda ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara 2025, Msemo alisema kuna umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya fedha kwa kutafuta washirika wapya na mbinu mbadala za kupata fedha.

“Serikali zetu zinapaswa kujitahidi kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka mataifa ya nje. Pia tunapaswa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha uwezo wetu wa kifedha,” alisema.

Msemo alielezea kuwa mabadiliko ya ghafla katika sera za misaada za Marekani, yakiwemo kuondolewa kwa misaada katika sekta muhimu kama elimu, afya na miundombinu, yameleta changamoto kubwa kwa nchi nyingi Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Hatua za haraka zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mgao wa bajeti kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa programu muhimu, huku bajeti za miaka ijayo zikizingatia uendelevu wa miradi katika sekta hizo muhimu,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic nchini Manzi Rwegasira, alisema ili sekta binafsi ivutie uwekezaji, ni muhimu kwa serikali kuimarisha mazingira ya biashara kwa kuboresha mifumo ya kodi, kutoa dhamana kwa mikopo na kushirikiana katika uwekezaji kwenye miradi.

Naye, Naibu Mkurugenzi wa IMF Idara ya Afrika, Cathy Pattillo, alisema nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zina uwezo wa kuongeza mapato ya ndani, lakini kiwango cha ukusanyaji kodi kwa sasa bado kiko chini ya matarajio ukilinganisha na uwezo uliopo. Alisisitiza kuwa mapato ya ndani ni chanzo cha uhakika na endelevu cha maendeleo.

Mwakilishi wa IMF nchini, Sebastian Acevedo, amesisitiza umuhimu wa kuwa watumishi wenye ujuzi wa kutosha ili kuweza kufaidika na idadi kubwa ya watu barani Afrika ili kukabili changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazoibuka.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!