Home VIWANDAUZALISHAJI Afrika yashauriwa kuweka mikakati kukabiliana na mabadiliko ya sera za kiuchumi

Afrika yashauriwa kuweka mikakati kukabiliana na mabadiliko ya sera za kiuchumi

0 comments 125 views

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amezishauri nchi za Afrika kuweka mikakati ya kufanya uwekezaji na biashara ndani ya Bara la Afrika ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sera za kiuchumi zinazojitokeza hivi sasa duniani.

Dkt. Nchemba ametoa ushauri huo jijini Washington D.C, nchini Marekani wakati akichangia taarifa ya Mwaka ya utekelezaji ya majukumu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wakati wa Mkutano wa Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) wa Magavana wa Shirika hilo wa Nchi za Afrika Kundi la Kwanza (Africa Group I Constituency – IMF).

Alisema kuwa mabadiliko ya kisera yanayojitokeza hivi sasa duniani ikiwemo vikwazo vya kibiashara vinavyotolewa na mataifa makubwa kwa kuongeza ushuru na tozo mbalimbali, iwe ni chachu kwa nchi za Afrika kutafuta njia za kujiimarisha kiuchumi kwa kuweka mipango madhubuti katika bajeti za nchi na kuuziana bidhaa.

Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa hali ilivyo sasa inaonesha nchi za Afrika zinakuwa washindani wa kibiashara badala ya kuwa washirika hali inayotishia mustakabali wa kiuchumi wa nchi hizo.

Alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuangalia maeneo ya uwekezaji katika miundombinu mbalimbali ndani ya Bara hilo ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa muhimu za binadamu na sekta nyingine zitakazochangia kukuza ajira kwa wananchi wao pamoja na kuimarisha uchumi wa nchi hizo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa ufinyu wa ufadhili wa kimataifa, unaochochewa na kupanda kwa viwango vya riba katika nchi zilizoendelea kiuchumi na kuhama kutoka kutoa misaada na ukopeshaji wa masharti nafuu, kumezuia zaidi nafasi ndogo ya kifedha katika nchi hizi kujiletea maendeleo.

Aliongeza kuwa matokeo yake, kuyumba kwa uchumi mkuu kumeongezeka, uwezo wa kitaasisi umemomonyoka, na upatikanaji wa ufadhili wa masharti nafuu na wa soko umezidi kuwa na vikwazo, na kudhoofisha matarajio ya kufikia maendeleo yanayotarajiwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Botswna  Cornelius Dekop aliunga mkono ushauri wa Tanzania na kusisitiza kuwa uchakataji wa bidhaa ndani ya nchi za Afrika pamoja na ushirikiano wa kibiashara, utakuwa na tija kubwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!