Kampuni ya Helium One, inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi ya helium nchini Tanzania, imekamilisha zoezi la ulipaji fidia ya zaidi ya milioni 100 kwa wananchi waliopisha shughuli za maendeleo ya mradi huo.
Wananchi hao ni wa vijiji vya Itumbula, Lwatwe, Masanyinta, Mkonko na Muungano Wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Akizungumza Aprili 24, 2025 wakati wa ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari, Msimamizi katika maeneo ya utafiti na Uendelezaji wa Mradi huo, Emmanuel Ghachocha, alisema kuwa fidia hiyo imelipwa kwa mujibu wa sheria za nchi na imelenga kuwawezesha wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za utafiti na uchimbaji.
Kwa mujibu wa Ghachocha, mradi huo ulianza rasmi mwaka 2015 kampuni ya Helium One ilipoanzishwa nakufanikiwa kufanya shughuli zake za kitafiti ikiwamo utafiti kwa njia ya mitetemo na uchimbaji wa visima vya utafiti.
Kuanzia mwaka 2021 mpaka 2025 Kampuni ya Helium One imekwisha chimba visima vinne, ambapo mafanikio makubwa yalionekana kwenye visima vya Itumbula West 1 na Tai 3 vilivyogundulika kuwa na mkusanyiko mkubwa wa gesi ya helium.
Baada ya kufanyika majaribio (Extended Well Testing) Kisima cha Itambula 1 ilionesha kuwa na mkusanyiko wa gesi hiyo ya helium yenye kiwango cha asilimia 7.9%.
Utafiti wa kina uliofuata pia ulionesha uwepo wa mkusanyiko wa gesi hiyo ya helium kwa kiwango cha asilimia 5.5 juu ya ardhi ikitokea kisimani.
“Mradi huu unatarajiwa kudumu kwa takribani kipindi cha zaidi ya miaka 10 ya uendelezaji na uzalishaji wa gesi hiyo,” alisema Ghachocha.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe, Mjiolojia Chone Malembo, alisema kuwa Songwe ina nafasi kubwa ya kuwa kinara wa uzalishaji wa gesi ya helium nchini, jambo ambalo litaongeza mchango wa mkoa huo katika Pato la Taifa kupitia sekta ya madini.
Ameeleza kuwa kwa sasa kinachosubiriwa ni Serikali kutoa leseni ya uchimbaji kwa kampuni hiyo baada ya kukamilika kwa utafiti ambao umeonesha uwepo wa gesi hiyo katika eneo hilo.
Helium ni gesi adimu kupatikana hapa duniani inayotumika katika teknolojia ya kisasa, huduma za afya, utafiti wa anga na sekta ya ulinzi ambayo mpaka sasa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa gesi hiyo ni Marekani, Urusi, Qatar, Saudi Arabia na Algeria na sasa Tanzania.