Home VIWANDAUZALISHAJI Serikali yaunda timu kuinua wachimbaji wadogo

Serikali yaunda timu kuinua wachimbaji wadogo

0 comments 187 views

Timu ya wataalamu ya kuishauri Wizara ya Madini juu ya kuwainua wachimbaji wadogo kiuchumi kupitia uchimbaji wenye tija imeundwa rasmi ikishirikisha wataalamu kutoka taasisi za umma na binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma Aprili 09, 2025 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameeleza majukumu ya timu hiyo kuwa ni pamoja na kupendekeza namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wazawa ili kuongeza tija ya uzalishaji madini, kupendekeza na kuendeleza wazo la uundwaji wa benki ya wachimbaji wazawa hapa nchini.

“Timu hii tuna imani itatuletea majibu baada ya mwezi mmoja, ni dhamira ya Rais kuona mchimbaji mdogo wa Tanzania anasimama anakuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha nchi yetu inapata manufaa makubwa na kujenga uchumi imara kupitia sekta ya madini,” amesema Waziri Mavunde.

Baadhi ya wajumbe wa timu iliyoundwa na serikali.

Lengo la timu hiyo ni kuhakikisha uchimbaji mdogo nchini unakuwa endelevu na unaendelea kuendeleza mchango wake katika sekta ya madini kupitia ajira na shughuli mbalimbali zinazofanyika kupitia miradi ya madini.

“Kutokana na umuhimu wa Sekta hii ndogo ya uchimbaji madini mdogo, naomba nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Sera yetu ya Madini ya Mwaka 2009 imeweka bayana kuwa, mkakati wetu ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini kwa kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kisasa sambamba na kuhakikisha wanakuwa na taarifa za kutosha za kijiolojia katika maeneo yao ya uchimbaji, kukuza mitaji yao, utaalamu pamoja na utunzaji wa mazingira.

Lengo jingine ni kuangalia namna ya kuwafanya wachimbaji wadogo wanakuwa na uwezo wa kuendesha uchimbaji utakaowafanya kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wachimbaji wakubwa.

Jukumu jingine ni kupendekeza uanzishwaji wa Mfuko wa madini utakaosaidia uendelezwaji wa shughuli za wachimbaji madini wazawa hapa nchini.

Timu hiyo inashirikisha wajumbe kutoka FEMATA, Wizara ya Madini, Benki ya NBC, GST, Tume ya Madini na TAMISA.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!