Home VIWANDAUZALISHAJI Tanzania yatoa rai nchi zilizoendelea kupunguza gharama za mikopo

Tanzania yatoa rai nchi zilizoendelea kupunguza gharama za mikopo

0 comments 131 views

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa nchi zilizoendelea kupunguza gharama za mikopo na kutoa muda mrefu wa kulipa madeni ili kuziwezesha nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika kutekeleza miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo jijini NewYork nchini Marekani, wakati akichangia mada katika Jukwaa la Ufadhili wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2025 (ECOSOC Forum on Financing for Development Follow-Up (FfD Forum), linalofanyika Makao Makuu ya Umoja huo.

Alisema kuwa mbinu za utoaji wa viwango vya mikopo zinapaswa kubadilika ili kuakisi kwa usahihi uwezo wa kweli wa nchi zinazoendelea kulipa madeni na kuhimiza matumizi zaidi ya fedha mchanganyiko (blended finance), upanuzi wa dhamana za hatari kutoka kwa Benki za Maendeleo ya Kielelezo (MDBs), na utekelezaji wa mipango ya uwazi wa madeni ili kusaidia kupunguza gharama za hatari zinazoonekana.

Dkt. Nchemba alipongeza juhudi zinazofanywa na mataifa pamoja na taasisi za fedha zinazokopesha kwa kuboresha upatikanaji wa mikopo nafuu lakini kwa nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, inakwazwa na viwango vikubwa vya gharama za mikopo na ulipaji wa madeni husika unaoathiri bajeti za nchi hizo.

Alipendekeza masuala matatu ya kufanyiwa kazi ikiwemo upatikanaji wa mikopo nafuu, kuongeza kasi ya kurekebisha muundo wa ulipaji madeni, kuwezesha upatikanaji wa mikopo mchanganyiko (blended finance) inayozingatia mahitaji pamoja na kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumzia umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi, Dkt. Nchemba alisema kuwa uwekeza wa sekta binafsi ni muhimu ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia kwa kujenga uchumi himilivu, jumuishi na kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma kimaendeleo.

Alishauri kuimarisha majukwaa ya kuwezesha uwekezaji ambayo yanaunganisha fursa na mitaji ya kimataifa, kuchochea athari chanya, na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma na kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na washirika wote kufungua uwekezaji binafsi kwa maendeleo jumuishi na endelevu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!