Hospitali ya CCBRT kupitia kitengo chake kipya cha afya ya uzazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete wameandaa chakula cha usiku cha hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kutoa huduma ya uzazi salama kwenye kitengo hicho.
Fedha hizo zitasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito walioko katika mazingira magumu na uzazi hatarishi.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT Brenda Msangi amesema “Kitengo hiki kina miundombinu maalum ya kuwahudumia wanawake wajawazito wenye ulemavu, wenye historia ya fistula na mabinti wanaopata ujauzito wakiwa na umri mdogo ili kuhakikisha wanawake wote wanapata huduma ya uzazi salama.
CCBRT kupitia kitengo hiki kina dhamira ya kuunga juhudi za serikali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na kuzuia ulemavu.”
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo itakayofanyika Jumamosi jioni tarehe 7 Mei, 2022, katika hoteli ya Serena Dar es Salaam anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mheshimiwa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Discussion about this post