Home Featured UNESCO na Ireland kushirikiana na Serikali kufanikisha Africa Code Week Tanzania

UNESCO na Ireland kushirikiana na Serikali kufanikisha Africa Code Week Tanzania

0 comment 111 views

SERIKALI ya Tanzania imeishukuru UNESCO na serikali ya Ireland kwa kufadhili programu ya kuwaendeleza vijana wa kitanzania kidigitali.

Programu hiyo, Africa Code week In Tanzania, imelenga kuwezesha vijana sio tu kujua dunia ya digitali lakini pia kuwa na uwezo wa kubuni na kutengeneza programu mbalimbali zinazogusa teknolojia ya digiti.

Akizungumza wakazi wa uzinduzi wa programu hiyo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Mh.William Ole Nasha alisema msaada huo wa serikali ya Ireland  ni muhimu kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata mafunzo ya tehama ili kusaidia katika mipango ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh.William Ole Nasha akizungumza na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Ole Nasha  alisema pamoja na kushukuru Ireland kwa kukubali kudhamini programu hiyo aliwasifu COSTECH na programu yake ya atamizi ambayo inachochea fikira za vijana katika matumizi na maendelelo ya teknolojia hasa upande wa digiti.

Alisema kitendo cha Ireland kusaidia programu hiyo inaamananisha kwamba inasaidia taifa la Tanzania kujenga uwezo wa matumizi ya teknolojia katika dunia ya viwanda na kuwawezesha vijana kutengeneza uwezo wa kujiajiri.

Awali katika uzinduzi huo Balozi wa Ireland nchini, Mh. Paul Sherlock alisema nchi yake imeamua kutoa msaada huo kutokana na kuelewa umuhimu wa kuendeleza vijana ambao ndio wajenzi wa uchumi wa taifa hili kwa miaka mingi ijayo.

Balozi wa Ireland nchini, Mh. Paul Sherlock akitoa salamu za serikali ya Ireland wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Alisema wanaamini kwa kuwa na vijana wengi wenye uwezo wa teknolojia watakuwa wamesaidia kuleta mapinduzi makubwa ya viwanda na pia kutengeneza idadi kubwa ya vijana wenye uwezo mkubwa wa kufanya shughuli zao kisayansi hasa kwenye upande wa uzalishaji.

Alisema kwa miaka ijayo, dunia itategemea zaidi teknolojia ya dijiti kufanya utatuzi mbalimbali wa masuala muhimu yanayohusu uchumi na jamii hivyo vijana zaidi ya milioni 15, wanaotarajiwa kuwapo nchini ifikapo mwaka 2030 watakuwa  ni nguvu kubwa kwa nchi ya Tanzania kama watakuwa wanakwenda sambamba na teknolojia ya digiti.

Alisema kwa kuielewa tehama vijana wengi watakuwa wametanzuka na changamoto ya ajira kwani watakuwa wabunifu na wenye uhakika wa kile wanachokitaka katika maisha ya kisasa.

Alisema ni matumaini yake kwamba vijana watatumia programu hiyo vyema kuhakikisha kwamba wanatoka kiushindani.

Awali ilielezwa kuwa mradi huo ulioanza mwaka 2016 kwa mwezi mmoja ujao utafunza walimu 500 ambao watatumika kusambaza maarifa ya code katika mashule mbalimbali, elimu ambayo itatumika kutatua matatizo ya msingi ya jamii.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa SAP Ireland, Bw. Liam Ryan amesema kwamba tangu mwaka 2016 ilipoanzishwa Africa Code Week zaidi ya watu 50,000 wamefundishwa na  zaidi ya watu milioni 1 wameanza kuifuatilia katika utekelezaji wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa SAP Ireland, Bw. Liam Ryan akizungumzia wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Alisema wamefurahishwa na mwitikio wa serikali ya Tanzania na anaamini kwamba kwa kuwezesha mafunzo hayo, tehama itafunguliwa kwa mapana yake.

Hata hivyo alisema kwamba wakati umefika wa kuingiza code katika mitaala ili itumike kunoa bongo za vijana ambao ndio dira ya miaka ijayo.

Wakati huo huo Mwalimu Miraji Kunoana kutoka shule ya sekondari ya Twiga alisema ni vyema serikali ikafikiria kuingiza masomo hayo katika mtaala kwa kuwa yatachangamsha akili ya vijana na kunoa bongo zao katika dunia ya digitali.

Mwalimu Miraji Kunoana kutoka shule ya sekondari ya Twiga akitoa ushuhuda wa Programu ya Africa Code Week ilivyokuwa msaada kwa wanafunzi wa shule yake wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa CSR EMEA na Africa Code Week Global Lead wa SAP Ireland, Bi. Claire Gillissen-Duval.

Alisema mafunzo ambao wameyapata yanawawezesha kufikiria nje ya boksi na kutengeneza chochote wanachotaka katika ubunifu wa teknolojia ikiwamo uumbaji wa vikaragosi na vitu vya kufundishia.

Mwanafunzi aliyefaidika na awamu ya kwanza ya mafunzo hayo Juliet Sewava  kutoka Shule ya sekondari ya Tambaza, alishukuru kwa  wafadhili wa mradi huo kwani wameweza kutengeneza uwezo wa kiteknolojia na ubunifu.

Mwanafunzi aliyefaidika na awamu ya kwanza ya mafunzo ya CODE, Juliet Sewava kutoka Shule ya sekondari ya Tambaza akitoa shukrani kwa wafadhali na ujumbe kwa serikali kupitia Wizara ya elimu wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Anasema wanaweza kwa sasa kutengeneza michezo mbalimbali ikiwemo ya vikaragosi kwa kutumia Code.

Wakati huo huo Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Habari UNESCO nchini, Nancy Kaizilege alisema kwamba mradi huo umelenga kuwezesha vijana kuwa jukwaa la mabadiliko katika matumizi ya tehama kwa manufaa yao na jamii.

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Habari UNESCO nchini, Bi.Nancy Kaizilege akitoa salamu za UNESCO YouthMobile wakati wa hafla mchapalo ya uzinduzi wa Programu ya Africa Code week Tanzania iliyofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Alisema UNESCO Youth Mobile imeungana na SAP na wafadhili wengine kuendesha kwa mwaka wa tano  Africa Code Week (ACW) kuhakikisha kwamba wanasambaza elimu ya code ili kuwawezesha kukuza zaidi ushiriki wao katika dunia ya teknolojia.

Alisema kuanzia mwaka 2015, zaidi ya watoto milioni 4.1  wameshiriki katika makongamano hayo na kwamba mwaka huu tukio kama la  Dar es Salaam katika bara la Afrika wanatarajia kufikia vijana milioni 1.5.

Huku asilimia 43 ya wakazi wake wakiwa na uwezo wa intaneti ukuaji wa teknolojia utabadili maisha ya wananchi wengi katika bara la Afrika na kutengeneza nafasi ya ajira.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter