Home BIASHARA Vitu vya kuzingatia katika biashara ya vifaa vya ujenzi

Vitu vya kuzingatia katika biashara ya vifaa vya ujenzi

0 comment 1.8K views

Kila siku watu wanajenga huku wengine wakiziboresha nyumba zao. Ni rahisi kupata mafanikio makubwa kupitia biashara ya vifaa vya ujenzi maarufu kama “Hardware” vilevile ni rahisi kwa biashara hiyo kufa ikiwa mfanyabiashara hana mpango madhubuti wa kuifikisha mbali.

Ikiwa unataka kufanikiwa katika biashara hii ni muhimu kuzingatia yafuatayo:

Soko

Ni muhimu kuelewa soko kabla ya kuwekeza fedha katika biashara yoyote. Kwa upande wa duka la vifaa vya ujenzi ni muhimu kuchagua maeneo yanayokua kwa kasi ili kupata wateja kwa urahisi.

Pia ni lazima kuchanganua udhaifu, nguvu, fursa na hatari zilizopo ikiwa utaanzisha biashara hii. Hakikisha unajua eneo zuri la kuanzisha biashara na kupata wateja kwa urahisi, kuwajua na kuwatathimini washindani ambao tayari wapo sokoni, kiasi cha fedha utakachohitaji.

Pia zingatia udhaifu wa washindani wako na utumie ipasavyo kuanzisha biashara itakayowahamasisha wateja kuja kununua bidhaa kwako.

Wekeza katika bidhaa zinazolipa

Ni dhahiri kuwa ili kuweza kuanzisha biashara ya vifaa vya ujenzi na ikasimama imara unahitaji kuwa na mtaji wa kutosha. Hivyo ili kuweza kuanza kujipatia faida haraka, zingatia bidhaa zinazouzika haraka zaidi na kuwekeza fedha zaidi.

Kwa mfano bidhaa ambazo huuzika kwa kasi zaidi katika maduka ya hardware ni pamoja na mabati, misumari, marumaru, vifaa vya milango, simenti nk.

Wafanyabiashara wengi huanza kuuza bidhaa hizi kwanza na kupanua biashara baadae baada ya kupata faida.

Hivyo kulingana na mtaji wako utachagua vifaa gani vya kuanzia navyo na kadri biashara inavyokua ndio unaweza kuongeza vifaa zaidi.

Usimamizi

Biashara yoyote inahitaji usimamizi, kuna ule msemo usemao mali bila daftari, huisha bila habari.

Ni muhimu kutengeneza mpango madhubuti kusimamia mapato, matumizi na shughuli zote zinazoendelea ili kuweza kujua faida na hasara zinazotokea na nini cha kufanya ili kubadilisha mambo yote yanayotokea na kuepuka hasara zinazotokana na wizi au uzembe wa wafanyakazi.

Kwa mfano kwa kuanza unaweza kuweka utaratibu wa kufanya mahesabu ya kina kila mwisho wa mwezi na mtaalamu, pia kulingana na uwezo wa biashara yako unaweza kuajiri mtaalamu kwa muda mfupi kila unapokuwa unahitaji huduma ili kupunguza gharama.

Ni muhimu kuwa na huduma bora kwa wateja, kuweka bei rafiki katika bidhaa zako, kutengeneza mahusiano mazuri na wateja ili kuhakikisha wanaitangaza biashara yako kwa ndugu jamaa na marafiki zao.

Vilevile hakikisha bidhaa zako zinaendana na wakati ili kuwahamasisha watu wengi hasa wale wanaopendelea kufanya mabadiliko kila baada ya muda.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter