Home AJIRA Faida za  ushirikiano kazini

Faida za  ushirikiano kazini

0 comment 438 views

Ili kampuni au biashara yoyote iweze kupata mafanikio makubwa kuna umuhimu wa kuwepo na ushirikiano baina ya wafanyakazi ili kurahisisha ufanisi wa kazi kama timu. Siku zote ushirikiano huwahamasisha wafanyakazi kuwa wabunifu zaidi jambo ambalo hupelekea uzalishaji kuongezeka na mwisho wa siku kuleta mafanikio kutokana na mahusiano mazuri baina ya wafanyakazi.

Kufanya kazi kwa ushirikiano na katika timu hurahisisha ufanisi wa kazi, na kusababisha kazi zifanyike kwa uharaka zaidi kuliko kila mfanyakazi akifanya kazi pekeyake. Pia kutokana na ushirikiaji wafanyakazi huwajibika na kupata motisha zaidi.

Kwamfano, si kila mfanyakazi huwa na ujasiri wa kuwasilisha mada au hoja mbele ya watu. Hivyo kupitia timu na ushirikiano kila mfanyakazi anaweza kutumia ujuzi  na talanta zake kuhakikisha mada inawasilishwa kiukamilifu, inaweza kuwa baadhi ya wafanyakazi wanauelewa zaidi wa masuala ya kiufundi lakini hawana ujasiri wa kuongea mbele ya watu hivyo watu hao wanaweza kujikita zaidi katika uandaaji wa nyaraka zote zinazohusu ufundi ili kuweza kuwarahisishia wafanyakazi wenye ujuzi na ujasiri wa kuwasilisha mada mbele za watu.

Ushirikiano hufanya watu wafikirie zaidi, waeleze mawazo yao kwa usawa na mwisho kujua uwezo na wa wafanyakazi wengine pamoja na mapungufu waliyonayo. Inaelezwa kuwa siku zote mawazo ya watu wawili au zaidi huwa na nguvu zaidi kuliko mawazo yanayotoka kwa watu mtu mmoja.

Wafanyakazi wakishirikiana, kimsingi hujifunza mambo mapya baina yao. Hiyo itapelekea wafanyakazi kujenga utamaduni wa kujifunza ili kuweza kufanya kazi zao kwa umahiri zaidi ili kuleta maendeleo katika kampuni au biashara.

Ikiwa wafanyakazi watashirikiana itakuwa rahisi kutekeleza mambo mbalimbali ya kikazi katika muda mchache. Changamoto au kazi ambazo zingeweza kufanywa miezi mingi na mtu mmoja zinaweza kufanywa masaa kadhaa ikiwa wafanyakazi watashirikiana. Hii huepusha biashara au kampuni kufanya mambo nje ya muda au kuchelewesha bidhaa au huduma kwa wateja.

Kama mmiliki wa biashara au kampuni makini, ni muhimu kuwahamasisha wafanyakazi kuhusu ushirikiano ili kuweza kupata matokeo mazuri kutoka kwa wafanyakazi hao. Pia hakikisha wafanyakazi wanapata teknolojia stahiki ili kuweza kurahisisha ufanisi wa kazi hii itaongezea motisha ya kufanya kazi badala ya kupoteza muda katika mambo ambayo yanaweza kufanyika kwa teknolojia.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter