Home BIASHARA BIASHARA YA MIWA NA FAIDA YA JUISI YAKE

BIASHARA YA MIWA NA FAIDA YA JUISI YAKE

0 comment 325 views

Biashara ya kutengeneza juisi ya miwa imekuwa maarufu sana katika mikoa mbalimbali hapa Tanzania. Hii inatokana na kinywaji hicho kuwa na manufaa mengi katika mwili wa binadamu. Moja kati ya kazi kubwa za juisi ya muwa ni kusafisha mkojo, figo na kutibu homa ya manjano.

Vile vile, juisi ya miwa ni kiburudisho ambacho hukata kiu hasa wakati wa joto. Pia miwa ni jamii ya tunda lenye alkali hivyo lina uwezo wa kupambana na saratani hasa ile ya kibofu cha mkojo na saratani ya maziwa. Sukari halisia ni nzuri kwa mwili kwani ina virutubisho na madini kwa wingi.

Miwa ina faida nyingi kiafya. Juisi ya miwa inafahamika na wataalamu wa afya kwa kuwa na uwezo wa kuupa mwili nguvu kwa sababu ya ‘glucose’ iliyopo. Kijiko kimoja cha juisi ya miwa, kina kalori 11. Madini halisi na vitamin zinazopatikana katika sukari ni kama phosphorus, calcium, madini ya chuma na potassium.

Miwa ina upekee wake kwani ina uwezo wa kuongeza maji mwilini, inaupooza mwili na kuupa nguvu.

Biashara ya juisi ya miwa ni moja kati ya biashara ndogo inayoweza kuanza na mtaji mdogo lakini ikakuletea faida kubwa kama mjasiriamali kulingana na uhitaji wake. Ili kuanza biashara hii mambo yafuatayo ni ya msingi kuzingatia:

1) Mashine ya kukamua miwa – Tsh 300,000-400,000

2) Glasi nzuri za ujazo tofauti – Tsh 20,000

3) Chujio – Tsh 5,000

4) Beseni – Tsh 8,000

6) Ndoo 2 – Tsh 10,000

7) Jaba kubwa la uchafu – Tsh 12,000

8) Mtaji wa kununua miwa –Tsh 50,000

9) Tolori la kusafirisha – Tsh 60,000

10) Vifaa vingine – Tsh 40,000

Jumla ya mtaji wa kuanzia Tsh 645,000/=

Muwa mmoja unaweza ukatengeneza lita 4 za juisi na muwa mmoja unaweza ukaununua kwa Tsh.300/=  kwa bei ya jumla. Lita moja ya juisi utauza 1,000/= hivyo kwa muwa mmoja unatengeneza Ths 4,000/=.

Mjasiriamali anaweza akaongeza ubunifu kwa kuongeza tangawizi au limao katika juisi yake ya miwa ili kuongeza ladha. Biashara hii ni nzuri hasa inapofanyika sehemu yenye mzunguko wa watu wengi kama stendi ya mabasi, masoko, n.k

CHANGAMOTO

  1. Changamoto zinazomkabili ni upatikaji wa bidhaa hiyo kwa msimu huku baadhi ya watu kutoamini maji anayotumia kutengenezea juisi kama ni salama kwa afya zao.
  2. Serikali imepiga marufuku vinywaji visivyo pimwa na TBS hivyo wakati mwingine ni usumbufu kwa mjasiriamali mdogo wa biashara ya juisi ya miwa.
  3. Wajasiliamali wa biashara hii wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa mazingira bora ya kufanyia kazi zao. Mfano uwepo wa wadudu kama nzi na nyuki mahali zinapofanyika biashara hizi.

Kulingana na faida itokanayo na utengenezaji na uuzaji wa bidhaa hii, mjasiriamali anashauriwa kuanza kidogo kidogo huku akiwa na malengo ya kukuza biashara hiyo kufikia usindikaji.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter