Home FEDHAMIKOPO UMASIKINI USIWE KIGEZO CHA KUKOSA ELIMU

UMASIKINI USIWE KIGEZO CHA KUKOSA ELIMU

0 comment 112 views

Ili kufanikisha masomo yao ya elimu ya juu, wanafunzi wengi hutegemea kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Kutokana na hali ya chini ya kiuchumi, watanzania wengi huchukulia bodi hii kama suluhisho pekee ili kufanikiwa kumudu gharama mbalimbali zinazokuja baada ya kuanza masomo yao vyuoni. Lakini sio wote wamekuwa wakibahatika na kufadhiliwa. Wengi wameendelea kuachwa nyuma katika hili hivyo kushindwa kujiendeleza kielimu hali ambayo inawaweka katika mazingira magumu kimaisha.

Mfumo wetu wa elimu umekuwa kikwazo kwa vijana wengi wasio na uwezo wa kumudu gharama kubwa za elimu ya juu. Kutokana na masharti ambayo siyo rafiki kwa wengi, kundi kubwa la vijana wameendelea kukosa haki yao ya msingi ya elimu kwa sababu tu hawana uwezo kifedha. lakini kwanini mwanafunzi akose elimu eti kisa ni maskini? Vipi kuhusu mchango wake katika kujenga Tanzania mpya ya viwanda? Miaka mitano ijayo vijana hawa watakuwa katika hali gani kiuchumi? Kwanini basi kusiwe na suluhisho mbadala la kusawaidia watu hawa?

Kila mtu anayo haki ya kupata elimu bila kujali uwezo alionao kiuchumi. Kwa kuwanyima fursa za elimu vijana, wataalamu tutawapata wapi? Vijana hawa watajikwamua vipi na hali ngumu ya maisha kama hata mikopo ya elimu ni mtihani? Wabaki tu mitaani bila kazi wala ajira kwa sababu tu walishindwa kugharamia elimu yao ya juu?

ADVERTISEMENT

Mwezi Agosti mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru alisema bodi hiyo imejipanga kutoa mikopo kwa wanafunzi zaidi ya 30,000 kwa mwaka wa masomo 2019/2020 huku kati yao asilimia 40 wakiwa wanafunzi wa masomo ya afya, sayansi ya elimu na hesabu. Mara nyingi wengi wanaojikita katika masomo ya sayansi hujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kupata mikopo kutoka katika bodi hiyo. Lakini kwa mwanafunzi asiye na historia na masomo ya sayansi nafasi yake ya kupata mkopo ikoje? Fani anayotegemea kusoma haina thamani kama zilivyo hizo nyingine? Hana mchango wowote katika kujenga taifa?

Ni kweli kwamba tasnia zinazotokana na masomo ya sayansi hazichaguliwi na wanafunzi wengi hivyo serikali kupitia bodi ya mikopo huweka mazingira mazuri kwa wachache wenye dhamira ya kusoma masomo hayo na njia moja ya kufanya hivyo ni kuwapatia mikopo. Lakini katika kufanya hivyo ni vizuri kama wanafunzi wengine hawatasahaulika. Kuwe na utaratibu ambao utawawezesha na wao kupata mikopo hiyo ili wapate elimu. Kila mmmoja wetu ana haki ya kujiendeleza kielimu hivyo wanafunzi wote kwa pamoja wawezeshwe katika hili ili wapate fursa ya kutimiza ndoto zao.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter