Home BIASHARA Jinsi ya kutengeneza bajeti inayofanya kazi

Jinsi ya kutengeneza bajeti inayofanya kazi

0 comment 127 views

Watu wengi hasa wa daraja la chini na kati huwa na nia ya kutengeneza bajeti lakini ni wachache sana huweza kufanyia kazi nia yao na kutengeneza bajeti inayofanya kazi na kuweza kuleta mabadiliko katika matumizi yao kwa mwezi, miezi sita hadi mwaka mzima.

Watu wengi hufikiri kuwa bajeti ni kwa ajili ya wale watu wanaoishi kutokana na malipo ya kila mwezi au wale wasio na fedha lakini hii sio kweli. Bajeti ni muhimu na inapaswa kila mtu awe nayo. Tajiri, masikini, na hata watu wa daraja la kati. Kuwa na bajeti kutakusaidia kuboresha hali yako kifedha na kutimiza malengo yako.

Kuandaa bajeti inaweza kuwa sio jambo la kufurahisha lakini ni muhimu kulifanya ili kuweza kudhibiti mtiririko wa fedha zako na kupunguza matatizo na vikwazo.

Fuata vidokezo vifuatavyo kutengeneza bajeti nzuri itakayoleta mabadiliko chanya.

Bajeti zinawasaidia watu kusimamia fedha zao vizuri na kwa urahisi. Mhusika anakuwa na kumbukumbu ya mapato na matumizi. Kuwa na bajeti ya mwezi kutakusaidia kujua ni kiasi gani unaweza kutumia katika kila kipengele, kiasi gani unaweza kufanya nacho kazi, na maeneo gani yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi kati ya mambo mengine. Bajeti zimewasaidia watu kufikia malengo yao, kulipa madeni na kutengeneza fedha zaidi.

Lazima utengeneze bajeti katika vifaa vya kieletroniki au katika karatasi? Hii inategemea na mtu anachoona kinamfaa. Kutumia karatasi kufanya bajeti si jambo baya lakini kutumia vifaa vya kieletroniki hurahisisha kufanya mabadiliko. Tumia njia ambayo ni rahisi kwako kwa sababu haijalishi unaorodhesha bajeti yako wapi jambo la muhimu ni kuhakikisha unaifuata. Baadhi matoleo yanayotumika kuweka bajeti katika mifumo ya kieletroniki ni pamoja na Spreadsheet, Mint, Personal Capital nk.

Unatakiwa kufuatilia mapato na matumizi yako. Jambo la msingi ni kutengeneza bajeti yenye uhalisia. Ili kujua fedha zako zinatoka wapi na kwenda wapi ni muhimu kukusanya risiti zako zote, nyaraka za benki na miamala ya mikopo. Anza kwa kufuatilia kila kitu kwa kipindi cha miezi miwili ili kujua matumizi yako yote (andika kiasi na kitu ulichokinunua) baada ya miezi miwili fanya tathmini ya matumizi yako, lazima utastaajabishwa na matokeo hayo. Kwa kupata matokeo hayo itakuhamasisha kuanza kufanya mabadiliko na kuepukana na matumizi yasiyo na msingi.

Katika kipengele cha mapato, hapa unatakiwa kuorodhesha vyanzo vyako vya mapato inaweza kuwa mshahara wa kazini, mali za kukodisha, kazi ya ziada nk. Ni muhimu kujua mapato yanaweza kupungua kwa kasi kutoka katika mwezi hadi mwezi hata kama unafanya kazi masaa yaleyale au hata kama unalipwa mashahara. Ni muhimu kuwa makini kuhusu muda unaolipwa. Utofauti wa kipindi unacholipwa unaweza kubadilisha kiasi unachopata kila mwezi.

Kwenye gharama za matumizi, ni muhimu kuweka gharama zako zote mfano Gharama za nyumba: malipo ya nyumba, kodi, matengenezo, bima,nk. Gharama za gari: mafuta kwa mwezi, marekebisho, bima, ada ya leseni nk. Gharama za chakula: vyakula vya kupikia, kula nje, vitafunio, nk.

Sio vibaya kumuhusisha mtu mmoja katika familia kuhusu bajeti hiyo ili kuhakikisha inasimamiwa ipasavyo. Pia mnaweza kukutana kila baada ya muda kuangalia mabadiliko yaliyofanyika na nini kifanyike zaidi ili kuhakikisha malengo yanatimia. Soi rahisi kwa bajeti kufanikiwa ikiwa watu wengine hawajui kama ipo.

Fanya mabadiliko inapobidi. Ni muhimu kupitia bajeti yako mara kwa mara. Inaweza kuwa mara moja kwa wiki, au mara moja kwa mwezi. Fanya kile ambacho unaona ni sahihi na kutokana na hali yako.

Ni muhimu kujua kuwa mambo mengi yanaweza kubadilika katika bajeti ikiwa ni pamoja na kipato, gharama za matumizi na hata malengo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter