Home Elimu JE,UNAJUA ATHARI NA FAIDA ZA KUAJIRI NDUGU AMA RAFIKI

JE,UNAJUA ATHARI NA FAIDA ZA KUAJIRI NDUGU AMA RAFIKI

0 comment 117 views

Ukuaji wa biashara hupelekea wamiliki wa biashara kuajiri wafanyakazi zaidi ili kuweza kukabiliana na mabadiliko hayo. Siku zote inashauriwa kuajiri watu ambao wana ujuzi au utaalamu wa kazi husika ili kuweza kupata matokeo chanya ambayo yataleta mafanikio zaidi katika biashara.

Mara nyingi inapofikia hatua hiyo watu wengi hufikiria kuajiri ndugu au marafiki kwa sababu wanawafahamu, wanahitaji ajira, na hata kwasababu wamekuwa wakiwasapoti tokea biashara husika inaanza. Ieleweke kuwa kuna watu duniani wameajiri ndugu au marafiki na kupata mafanikio makubwa na kuna watu wameajiri watu wao wa karibu na kupata changamoto nyingi katika biashara zao. Hivyo hapa chini nitaeleza faida na hasara za kuajiri watu wa karibu ili uweze kufanya maamuzi sahihi katika biashara yako:

Faida

  • Mchakato mzima wa kuajiri hufanyika katika muda mfupi, kwasababu unajua uzoefu wao, historia zao,mitizamo yao na hata tabia zao. Ambapo kwa kuajiri watu usiowafahamu hivyo vyote unakuwa hujui na huwa kuna itifaki zinazochukua muda kupata mtu ambaye anafaa katika ajira husika.
  • Ndugu na marafiki wanaweza kukubali malipo ya chini na hata kufuata ratiba isiyo rasmi ili kuweza kukusaidia kufanikiwa na hata kufikia malengo ya biashara.
  • Pia kwa kusaidia ndugu na jamaa inaleta picha nzuri , kwani mwisho wa siku hakuna mtu ambaye anataka kufanikiwa huku ndugu na marafiki wana hali mbaya.

Hasara

ADVERTISEMENT
  • Si rahisi kuweka mipaka na sheria kuhusu masuala binafsi na ya kazini kwasababu ndugu na marafiki ni watu ambao unakuwa nao kila siku, unajua mambo yanayohusu maisha yao ya kila siku. Kwa namna moja au nyingine kutakuwa na mkanganyiko wa maeneo hayo mawili hali inayoweza kupelekea changamoto katika biashara.
  • Watu wengi huajiri ndugu au marafiki kwasababu ya huruma. Hii inaweza kuleta shida mbeleni hasa kama ndugu huyo hana ujuzi au utaalamu unaotakiwa. Kwa namna moja au nyingine ukosefu wa ujuzi hupelekea matokeo yasiyoridhisha hali ambayo inaweza kusababisha ugomvi na hata kuharibu mahusiano baina ya ndugu au marafiki.
  • Ni rahisi kupendelea ndugu au rafiki katika mahali pa kazi. Hata kama utafanya kila kitu kwa usawa baina ya wafanyakazi wako lakini kwa namna moja au nyingine wafanyakazi wengine  wataona ndugu au rafiki yako anapendelewa. Hii inaweza kupelekea chuki, maadili ya chini na changamoto nyingine nyingi katika biashara.

Hivyo, baada ya kujua hasara za kuajiri watu wa karibu, ikiwa bado unataka kumuajiri ndugu au rafiki zingatia vidokezo hivi:

  • Hata kama mahojiano baina yako na mtu wako wa karibu hayatokuwa rasmi lakini ni muhimu kuomba Wasifu (CV) wake, na kutathmini uwezo na utaalamu walio nao ili kuweza kuamua kama kazi husika wataiweza na kwa asilimia ngapi.
  • Weka matarajio moja kwa moja ili kuepuka mifarakano mbeleni. Kama ambavyo ungefanya kwa mfanyakazi wa kawaida hakikisha ndugu/rafiki yako anajua sheria za kazi, malipo,faida(benefits), ratiba ya kazi, sera za kufuata na hata kuhakikisha anasaini mkataba au makubaliano.
  • Hakikisha unawasimamia watu wako wa karibu kutokana na utendaji wao wa kazi badala ya mahusiano mliyo nayo ili kuepusha maoni au mawazo ya upendeleo mahali pa kazi.

Mwisho wa siku, si lazima utoe ajira kwa watu wa karibu ili hali unajua kwa kufanya maamuzi hayo unahatarisha biashara yako. Unaweza kuwatafutia ndugu na marafiki ajira katika kampuni au biashara nyingine kulingana na uwezo pamoja na utaalamu walio nao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter