Home BIASHARA UNAFAHAMU LOLOTE KATIKA BIASHARA YA VITABU…

UNAFAHAMU LOLOTE KATIKA BIASHARA YA VITABU…

0 comment 110 views

Kila binadamu ana kile anachopenda kufanya ili kupata burudani na liwazo katika mwili wake. Wengine hupenda kutembea ufukweni na kupunga upepo, wengine hupenda kutoka sehemu za starehe na marafiki au wenzi wao na wengine hupenda kukaa nyumbani na kujisomea vitabu mbalimbali vikiwemo vitabu vya taaluma, hadithi, Afya, na vingine vingi.

Utumiaji wa vitabu kama sehemu ya kutuliza akili sio moja ya tamaduni kubwa sana katika jamii za kiafrika lakini bado matumizi ya vitabu yamezidi kuongezeka kutokana na uwepo wa shule na tassisi mbalimbali za kielimu.

Licha ya kuwepo uhitaji wa vitabu vya taaluma bado uwekezaji katika masuala ya maduka ya vitabu ni mdogo sana. Hii inatokana na kutowepo kwa mkazo mkubwa na hamasa kwa wafanyabiashara kuwekeza katika biashara hii. Ni jambo la kawaida kuzunguka Jijini Dar es salaam ukitafuta kitabu cha muhimu sana na ukazunguka hata maduka matano usipate kitabu hicho. Zaidi utaambiwa nunua Amazon kwa njia ya mtandao.

Kama yalivyo mahitaji mengine suala la vitabu ni muhimu sana katika maisha ya binadamu. Kati ya faida unazopata kwa kusoma vitabu mara kwa mara ni pamoja na kuongeza uwezo wa ufikiri,inasaidia kupunguza msongo wa mawazo,kuamsha akili,kuongeza maarifa, kuwa na uwezo wa kujua misamiati mingi ya lugha,kuwa na ujuzi mkubwa wa kuandika, kuwa mtu makini na mwenye mtazamo wa mbele pamoja na kuwa kama sehemu ya burudani.

ADVERTISEMENT

Basi kama una mtaji na haujui namna unavyoweza kuwekeza hili ni jambo kubwa na la muhimu kwako.  Kitu cha muhimu ni kuangalia mazingira na uhitaji wa watu wanaokuzunguka. Hivi hapa ni vitu unavyotakiwa kufanya unapotaka kuanzisha biashara ya kuuza vitabu vikiwemo vitabu vya biashara na ujasiriamali, uwekezaji, kilimo, afya, hadithi, viwanda na masuala mbalimbali yanayohusu maisha.

  1. Soko. Soko ni kitu cha muhimu sana unapotaka kuanzisha biashara hii. Unatakiwa kujua wateja wako ni akina nani na wanapendelea vitabu vya aina gani.Tengeneza wateja wako kwa mfumo wa kuangalia nini hasa uhitaji wao. Uchaguzi wa watunzi wa vitabu pia unaweza kukusaidia kuifanya biashara yako ikapendwa zaidi. Wafanye wateja wajue kuwa duka lako lina kila aina ya mahitaji wanayoyataka.Mfano unaweza kuwa na vitabu vya watoto, mapishi,mahusiano, masuala ya familia na maadili,. Pia toa ofa kwa wateja wako. Hapa yaweza kuwa kwa kuwapa kitabu kimoja kwa kila mteja atakayenunua vitabu kumi.
  2. Uchaguzi wa Vitabu. Tafuta vitabu vinavyoonekana kuwa na uhitaji wa mazingira uliyopo. Vitabu vinavyoakisi uhalisia wamzingira waliyopo. Kwa mfano uko mazingira yenye makazi ya watu basi ni vema kuangalia vitabu vinavyohusu malezi ya watoto au vitabu vinavyoburudisha watoto,. Vivyohivyo katika mazingira ya vyuo unatakiwa kuzingatia uhitaji wao pamoja na kungalia vitabu vinavyouzika kwa sana
  3. Taaluma au Ujuzi wa mauzo. Biashara yoyote inapofanyika lazima ihitaji mjuzi wa biashara hiyo. Japo ujuzi mwingine umekuwa ukitokea kutokana na uzoefu ambao mtu amechukua kujifunza katika biashara hiyo hiyo aliyoianzisha. Chukua muda wa kutosha kuongea na wateja wako kuhusu vitu wanavyopendelea kujua.
  4. Gharama. Moja ya vitu vinavyoathiri biashara nyingi za watu ni kutojua hali ya uchumi ya watu wanaoizunguka biashara yao. Siku zote bidhaa inayouzwa Mlimani City ikichukuliwa bidhaa hiyo hiyo ikauzwa Mbagala haiwezi kuwa bei sawa. Hii inatokana na bidhaa kupangwa kutokana na hadhi ya eneo. Vivyo hivyo chumba cha Oysterbay chenye mfanano na cha Manzese haviwezi kupangishwa kwa bei moja. Hivyo basi mfanyabiashara anashauri kujua hali ya uchumi ya watu wanaomzunguka na kuja na bei itakayokuwa rafiki kwao kuweza kununua.
  5. Zingatia sera ya kurudisha. Biashara nyingi zina sera na ofa ya kurudisha pale ambapo mnunuzi anakuwa hajaridhika nayo. Mfanyabiashara wa nguo anapoagiza sketi anajua kabisa kile kitu anachoagiza kuanzia ukubwa hadi rangi. Na endapo hatoridhishwa na bidhaa aliyotumiwa ana uwezo mkubwa wa kuirudisha kwa aliyemuuzia. Hii ipo tofauti kwa watunzi na wamiliki wa vitabu, hawa hawana hiyo sera, ni jambo la kawaida kukuta kitabu kilichonunuliwa mwaka 1992 hadi mwaka huu bado kipo dukani. Kikubwa ni kwamba kadri kitabu kitakavyozidi kukaa dukani ndivyo kitazidi kupoteza uhalisia wa mazingira yaliyopo na yajayo.

Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa inachukua hatua kadhaa kuhakikisha inaifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati, tumeshuhudia kuwepo kwa ongezeko kubwa la wageni katika sekta ya utalii na uwekezaji. Waandishi wengi wa Tanzania wamekuwa wakijikita zaidi katika kuandika vitabu vya simulizi za mapenzi badala ya kuangalia uhalisia wa mazingira yaliyopo.

Ni muda sasa wa kuamka na kuitangaza Tanzania. Sifa za Tanzania zimesambaa ulimwenguni kote lakini bado kuna watu wanahitaji kujua zaidi juu ya vitu vinavyoitofautisha Tanzania na nchi nyingine hasa vya kipekee na visivyoweza kuonekana sehemu nyingine duniani. Tuandike vitabu vitakavyoamsha hali na mazingira mazuri kwa wawekezaji wa nje kuvutiwa na hali ya mazingira yetu ili tuijenge Tanzania yenye maendeleo na ustawi kwa ajili ya kizazi cha leo na cha baadae.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter