Home Elimu MBINU BORA ZA KUFUGA SAMAKI

MBINU BORA ZA KUFUGA SAMAKI

0 comment 126 views

Ufugaji wa samaki ni moja kati ya shughuli zenye kuingiza kipato kikubwa kwa mjasiriamali endapo tu atakuwa na nia ya kufanya aina hiyo ya ufugaji, kwa sababu ili mtu aweze kufanikiwa katika shughuli yoyote jambo kubwa ni uthubutu. Ufugaji wa samaki ni gharama na unahitaji muda wa kutosha sambamba na umakini mkubwa sana. Watu wengi wameanzisha ujasiriamali huu lakini wameshindwa kufika mbali kutokana na kutojua mbinu bora za ufugaji huo wa samaki.

Rasilimali muhimu za kuwa nazo ili kufanikisha shughuli hii ni eneo la ardhi, maji, rasilimali watu na rasilimali fedha. Eneo la ardhi litaonyesha namna gani bwawa lako litakavyokuwa, aidha la kujengea na cement, kutandika plastiki au kuchimba na kulitumia hivyo hivyo. Bwawa huchimbwa/kujengwa kwa kuwa na sakafu yenye ulalo kiasi

Wapo samaki aina ya Sato (Tilapia), Kambale (African catfish) na wengine aina ya pangasius ambao hufugwa kwa wingi sana.

Zipo mbinu mbalimbali zitakazo kusaidia kuwa mfugaji bora wa samaki. Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na:

ADVERTISEMENT

i) Unahitaji samaki 7-8 katika mita moja ya mraba. Kwa maana hiyo kama una mita za mraba 600 basi unaweza kufuga samaki 4500. Haishauriwi kujaza samaki kwenye eneo dogo kwani itawasababishia ukosefu wa hewa ingawa zipo njia za kuweza kuongeza upatikanaji wa hewa kwenye mabwawa.

ii) Shauku na dhamira ya kweli ya ufugaji. Ni wazi kuwa dhamira ya kweli ni kitu muhimu sana unapotaka kufanya jambo lolote kwani bila kudhamiria basi huwezi kufanikiwa, matokeo ya kutokuwa na dhamira ni kukata tamaa pindi utakapokutana na changamoto ya aina yoyote lakini ukiwa umedhamiria utakuwa na uwezo wa kuzikabili changamoto na hivyo kujikuta ukifika mwisho wa safari yako huku ukiwa na mafanikio.

iii) Fanya tathmini ya rasilimali ulizonazo kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa samaki Tathmini hii inahusisha nguvukazi, rasilimali pesa, pamoja na umiliki wa eneo. Mkulima akiweza kujitambua na kutambua uwezo wa nguvukazi aliyonayo itakuwa ni rahisi kwake kumudu majukumu mbalimbali yaliyopo katika ufugaji, pia katika suala la kutambua ukubwa wa ardhi aliyonayo litamsaidia kujua idadi ya samaki anaoweza kufuga pamoja na kiasi cha fedha kinachohitajika.

iv) Chanzo endelevu cha mtaji kwa ajili ya mradi. Mfugaji anatakiwa kuwa na chanzo cha uhakika cha kujipatia mtaji wake ambacho kitakuwa ni endelevu ili asije akajikuta anakwama kupata pesa ya kununulia mahitaji pindi yanapohitajika na hivyo kumpunguzia ubora katika ufugaji wake. Mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka anawashauri wakulima wajiunge katika vyama mbalimbali vya kuweka akiba na kukopa (SACCOS) ikiwa ni pamoja na vikoba  ambavyo hutoa mikopo kwa riba nafuu na taratibu zake za marejesho hazina masharti magumu hivyo kumwezesha mfugaji kukopa kwa urahisi wakati wowote  anapokuwa na mahitaji ya fedha.

v) Uvumilivu na Uthubutu. Mfugaji mtarajiwa wa samaki anapaswa aelewe kuwa ufugaji wa samaki ni mradi kama ilivyo miradi mingine ambayo unaweza kuwekeza lakini faida yake isiweze kuonekana mara moja. Hapa mfugaji anatakiwa awe mvumilivu katika kipindi chote cha mwanzo cha ufugaji kwani hiki ni kipindi cha mpito ambacho kinaweza kumfanya asipate faida lakini akiwa mvumilivu baada ya mradi kukomaa basi atapata faida na inashauriwa mfugaji kutumia rasilimali za kifamilia katika hatua za awali ili kuepuka madeni katika kipindi cha mpito.

vi) Tathmini ya soko la bidhaa za samaki. Soko ni jambo muhimu sana katika suala la biashara kwani hilo ndilo litakalokuongoza na kukuwezesha kujua mahitaji ya watu pamoja na kupanga bei. Mfugaji hana budi kufanya utafiti na kuelewa ni kwa kiasi  gani biashara anayotaka kuifanya inakubalika katika jamii aliyopo kinyume cha hapo anaweza asifanikiwe, kutokana na biashara anayoifanya kutokuwa na soko au kutokubalika katika jamii inayomzunguka.

vii) Kujipatia maarifa ya msingi ya ufugaji. Kitu chochote ili uweze kukifanya kwa ufanisi ni lazima uwe na elimu au maarifa ambayo yatakuongoza katika utekelezaji. Mtu mwenye elimu ya biashara anayofanya anapata faida zaidi ukilinganisha na yule anayefanya bila kuwa na mwongozo. Katika ufugaji wa samaki vyanzo vya maarifa vinaweza kuwa ni majirani zako ambao ni wafugaji, taasisi za dini zenye miradi kama hiyo, ofisi za serikali na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter