Home AJIRA Waziri ataka wahitimu kufungua kampuni zao

Waziri ataka wahitimu kufungua kampuni zao

0 comment 125 views

Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amewashauri wahitimu kutumia elimu waliyoipata kujiajiri na kuajiri watanzania wenzao badala ya kutembea na vyeti kutafuta ajira.

Waziri Mwambe alitoa wito huo katika Mahafali ya 55 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Mimi ningetamani kusikia kila mmoja hapa anaanzisha kampuni yake, wewe uliyesomea uhasibu anzisha kampuni ya kutengeneza hesabu za makampuni mbalimbali, uliyesomea ukaguzi anzisha kampuni ya kukagua hesabu na hata waliosomea masoko hivyo hivyo,”  alisema Mwambe.

Amesema kuna fursa nyingi sana ambazo wahitimu wanaweza kuzitumia na kuwa na maisha mazuri wakiwa wabunifu kwani sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu na siyo serikali.

Waziri Mwambe amesema kazi ya serikali itakuwa kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa sekta binafsi ili kuiwezesha kuongeza uzalishaji, kuongeza tija ili hatimaye Tanzania iwe na uchumi mkubwa Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na duniani ikiwezekana.

Alikipongeza chuo cha CBE kwa kufanikiwa kupanda kwa hadhi ya ubora wa vyuo vikuu ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano.

Alisema hatua ya chuo hicho kupanda ndani ya muda mfupi kutoka nafasi ya 54 mpaka 14 ni jambo la kuigwa na la kujivunia na aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na chuo hicho kuhakikisha miundombinu yake inaboreshwa.

“Mmefanya kazi kubwa sana kuvuka kutoka nafasi ya 54 hadi nafasi ya 14 ndani ya miaka mitano si kazi ndogo, changamoto zote zilizosemwa hapa nimezichukua na ninawaahidi ushirikiano kuzitatua sitawaangusha kwasababu tunataka kuona CBE ikiendelea kutoa wahitimu bora,” alisema

Katika mahafali hayo, wahitimu 2,248 walitunukiwa astashahada, shahada na shahada za uzamili katika fani mbalimbali.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter