Shilingi bilioni 28 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa soko jipya la Kariakoo, Dar es Salaam.
Ujenzi huo unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, umekuja baada ya soko hilo kuteketea kwa moto uliotokea katika soko hilo la kimataifa Julai 10, 2021 jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amesema ukarabati na ujenzi wa soko hilo la gorofa 6 utaanza baada ya Tarehe 09 Disemba.
RC Makalla, ampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha hizo na kuwajali wafanyabiashara.
Aidha, RC Makalla amewaondoa hofu wafanyabiashara wa soko hilo wenye wasiwasi kuwa baada ya ujezi kukamilika watapangishwa watu wengine ambapo amesema wazawa watapewa kipaumbele.
Asema wahanga wa soko la kariakoo na soko dogo watapewa kipaumbele kurejea soko litakapokamilika.
Amebainisha kuwa tayari Mkandarasi wa kukarabati na kujenga amepatikana.
Baada ya tukio la moto huo, Rais Samia Suluhu Hassan aliviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliunda kamati ya kuchunguza tukio la moto ulioteketeza maduka na mali za wafanyabiashara katika Soko hilo Kuu na mnamo Julai 27, 2021 alipokea taarifa ya uchunguzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hayo, CP Liberatus Sabas na kuahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo.