Home BIASHARAUWEKEZAJI Rais Samia aita wawekezaji wa Oman

Rais Samia aita wawekezaji wa Oman

0 comment 155 views

Rais Samia Suluhu Hassan amewaita wafanyabishara wa Oman kuja kuwekeza nchini huku akiwahakikishia mazingira mazuri ya biashara na uwepo wa nguvu kazi ya kutosha.

Rais Samia ambae yupo nchini Oman kwa ziara yake ya kikazi ya siku tatu iliyoanza Juni 12, 2022 amesema zipo fursa tofauti ambazo wanaweza kuzitumia katika uwekezaji .

Akizungumza June 13, 2022 wakati akishiriki kongamano la wafanyabiashara nchini humo amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, madini, utalii na viwanda na kuwahakikishia soko la uhakika.

Rais Samia amesema endapo Oman itatumia fursa ya kuwekeza nchini itanufaika na soko kubwa ambalo Tanzania inaweza kulifikia.

“Sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, pia ni wanachama wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao kwa pamoja tunatengeneza idadi ya watu kuwa karibu ya milioni 500 ambalo ni soko kubwa,”

“Pia sisi ni wanachama wa soko huru la Afrika (ACFTA) hili linaongeza idadi ya watu na kufanya soko la watu kuwa 1.3 bilioni,” amesema Samia.

Amesema pia Tanzania ni geti la nchi zote za Afrika hivyo mtu anapofanya uwekezaji anaweza kufikia nchi nyingi zaidi.

Rais ameeleza kuwa karibu asilimia 67 ya watu wote nchini Tanzania ni vijana wenye uwezo wa kufanya kazi katika kampuni zitakazoanzishwa na uwekezaji utakaofanywa hivyo kuwahakikishia nguvukazi ya kutosha.

Akielezea kuhusu maendeleo ya miundombinu nchini Rais amesmea “tumewekeza katika reli ya kisasa ambayo inakatisha katikati ya Tanzania na kuunganisha Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mkifika huko mnaweza kuunganishwa na nchi nyingine za Afrika.”

“Najua kumekuwa na changamoto zinazokatisha tamaa lakini niko hapa, naenda kufanyia kazi yale yaliyotokea kabla na tunakwenda kufanya kazi pamoja na kufanya uwekezaji kati ya nchi hizi mbili,” alisema Samia.

Ameeleza kuwa licha ya sekta za kilimo, ufugaji na uvivu kuwa ni muhimu bado hazijaguswa ipasavyo.

Qais bin Mohammed Al Yousef ambae ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji nchini Oman amesema wako tayari kujadili ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na kuendeleza fursa ambazo Tanzania imezitaja.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter