Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia watumishi wa umma waliondolewa kazini kwa sababu ya vyeti feki, walipwe michango yao waliyochangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Rais Samia ametangaza hayo mjini Dodoma Oktoba 26, 2022 ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema utekelezaji wa kurejesha mafao hayo utaanza rasmi Novemba Mosi, 2022.
Profesa Ndalichako amesema “marejesho ya michango kwa watumishi hao yataanza kufanyika kuanzia tarehe moja, Novemba, na tungependa kwa kweli jambo hili likamilike ndani ya muda mfupi.”
Amesema ili kuwezesha malipo hayo kufanyika mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri na kuchukua nyaraka zote muhimu ambazo zinatakiwa.
“Niwaombe, wasiamkie kwenye Mifuko ya Jami, taratibu ni zilezile anatakiwa awe na picha mbili pasaport size awe na nakala za kibenki yaani akaunti iliyo hai malipo haya hayatolewi pesa taslimu yatafanyika kwenye benki, kwa hiyo lazima mtumishi husika aoneshe taarifa zake za kibenki lakini pia atatakiwa awe na kitambulisho cha taifa, kitambulisho cha kura au leseni ya udereva, ” amesema.
Amesema pia mtumishi atatakiwa kujaza hati ya ridhaa kwa aliyekuwa mwajiri wake.