Home BIASHARAUWEKEZAJI Mfumo wa umilikishwaji fukwe kupitiwa upya

Mfumo wa umilikishwaji fukwe kupitiwa upya

0 comment 122 views

Katika kurahisisha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa maeneo ya fukwe nchini kwa lengo la kukuza utalii, serikali imependekeza kupitiwa upya kwa mfumo wa umilikishwaji wa fukwe.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja  amesema hayo Novemba 24, 2022 jijini Mwanza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Nane la Maendeleo Endelevu lenye dhima ya usimamizi madhubuti wa fukwe kwa maendeleo endelevu.

Amesema “tunapendekeza mfumo wa umilikishwaji fukwe upitiwe upya ili ikiwezekana umiliki uhamishiwe katika wizara mojawapo kama Wizara ya Uwekezaji au Sekta ya Utalii.”

Masanja ameeleza kuwa kwa kufanya hivyo kutarahisisha uwekezaji na kutengeneza mazingira bora zaidi ya fukwe hizo.

Amesema pendekezo hilo linatokana na maoni ya kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kilichopitia fukwe na kugundua kuwa asilimia kubwa ya fukwe  zinamilikiwa na watu  binafsi lakini nyingine zinamilikiwa na Serikali za mitaa, hivyo kupelekea kutokuwa na uelewa wa pamoja juu ya uwekezaji katika maeneo ya fukwe.

Amebainisha kuwa changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi  ili kuweka uelewa wa pamoja juu ya uwekezaji katika maeneo ya fukwe na kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuweza kuzifikia fukwe kwa urahisi.

Amesema kikosi kazi hicho kilichoundwa mwaka 2016 kilitembelea mikoa kadhaa ikiwemo Lindi, Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Mtwara kwa lengo la kuzitambua na kuziainisha fukwe zilizopo katika maeneo hayo.

Ameeleza kuwa kikosi kazi kilileta mapendekezo ya kuzitambua fukwe na kuangalia umiliki wake sambamba na kuangalia jiografia zinazofaa kama zinawiana na masuala ya utalii.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter