Benki ya Dunia (WB) imewekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 7.2 sawa na takribani Sh. trilioni 16.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya 29 nchini Tanzania.
Kati ya miradi hiyo, miradi 24 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6.41 ni ya kitaifa na mingine 5 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 0.75 ni ya kikanda.
WB imeipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa WB anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, amesema hayo wakati wa mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye Mikutano ya Kipupwe ya WB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Dkt. Ngaruko, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Dunia katika ukanda huo, amesema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.
“Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa usimamizi mahiri wa masuala ya uchumi mpana, sio tuu kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana” amesema Dkt. Ngaruko.