Home BIASHARA Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kutembelea mikoa

Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kutembelea mikoa

0 comment 95 views

Kamati maalum ya kutatua changamoto za kibiashara nchini iliyoundwa na Waziri Mkuu Khasim Majaliwa Majaliwa imehitimisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kutoka sekta mbali mbali Jijini Dar es Salaam Mei 27, 2023.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dr.John Jingu amesema kuwa kamati hiyo imeshafanya kazi yake kwa asilimia sabini (70%) na sasa inatawanyika katika makundi mbalimbali katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwafikia wafanyabiashara waliopo katika maeneo hayo.

Dkt. Jingu amesema ikiwa ni siku ya tisa tangu kamati ianze kazi kuna baadhi ya changamoto za kiutendaji ambazo mpaka sasa zimeshatatuliwa kama mizigo ya baadhi ya wafanyabiashara iliyokuwa ikishikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeachiliwa na kusitishwa kwa vikosi vya operasheni za ukusanyaji kodi kwenye soko la Kariakoo.

“Wafanyabiashara wameshachukua mizigo yao na wengine wanaendelea kushughulikia jambo hilo ambalo limeleta matumaini kwa wafanyabiashara, tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa kwa wadau wetu na wote tunaowatembelea wanatuambia tusimwangushe mama’’ ameongeza Dkt. Jingu.

Kwa upande wake Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Hamis Livembe ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwajumuisha kwenye kamati hiyo jambo linaloonesha Serikali ya awamu ya sita ni sikivu.
‘’Mara nyingi tumekuwa nje ya vyombo vya maamuzi lakini kwa sasa tunashirikiana na Serikali kutatua changamoto za wafanyabishara nchini’’ amesema Livembe.

Kamati hiyo inatagawanyika katika kanda tano ambazo ni Kanda za nyanda za juu kusini (Mikumi, Iringa, Makambako, Mbeya na Tunduma), Kanda ya ziwa (Kahama , Mwanza na Sirari), Kanda ya Pwani (Zanzibar, Lindi na Mtwara) Kanda ya Magharibi (Kigoma na Kagera) na Kanda nyingine ni Kanda ya Kaskazini yenye Mikoa ya Arusha , Kilimanjaro na Manyara.

Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 14 ambapo wajumbe saba ni wawakilishi wa wafanyabiashara nchini na wajumbe wengine ni kutoka idara na Wizara mbalimbali zinazohusika na biashara nchini.

Soma: Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter