Home FEDHAMIKOPO Soko la ndani la mitaji kusaidia nchi za Kusini mwa Afrika

Soko la ndani la mitaji kusaidia nchi za Kusini mwa Afrika

0 comment 120 views

Nchi za Kusini mwa Afrika zinaangalia namna ya kuendeleza soko la ndani la mitaji kwa kutumia hati fungani ili kuziwezesha kupata mikopo ya ndani.

Hii ni kutokana na hali ya mikopo mingi ya kibiashara duniani kuwa ikipatikana kwa gharama kubwa.

Akizungumza jijini Arusha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara hiyo Japhet Justine, ameeleza hayo wakati wa Mkutano wa Wataalamu wa masuala ya uchumi na fedha wanaosimamia madeni ya nchi zao kutoka nchi 16 za kusini mwa Afrika.

Amesema nchi za kusini mwa Afrika zinaangalia namna ya kutumia soko au hati fungani za ndani ambazo ni za muda mfupi, wa kati na mrefu zinatoa nafuu kubwa kwa nchi za Afrika, kwa kuwa mikopo ya aina hiyo ni nafuu na haihitaji matumizi ya dola wala uwekezaji wa nje na haina shinikizo wakati huu ambao soko la dunia halifanyi vizuri.

“Duniani mikopo ya kibiashara inapatikana kwa gharama kubwa, hivyo mikopo ya ndani itakuwa sehemu ya hatua muhimu ya kuzisaidia nchi za Afrika kufanikisha ufadhili wa bajeti kwa ajili ya maendeleo yao”, amesema Justine.Justine ameeleza kuwa kuliendeleza soko la ndani la hati fungani kunatoa fursa kwa nchi za Afrika kufanya vizuri zaidi, ambapo Tanzania kwa sasa inapata mikopo ya zaidi ya trilioni saba kutoka soko la ndani ambayo husaidia kufanikisha bajeti Kuu ya Serikali.

Ameongeza kuwa zipo nchi ambazo zinafanya vizuri katika bajeti zao kwa kutumia fursa ya soko hilo ikiwemo Namibia ambayo zaidi ya asilimia 80 ya Bajeti yake inatokana na mikopo ya ndani kupitia hati fungani zake.

Amesema mkutano huo utajadili na kuchambua aina ya hati fungani za ndani zinazotolewa huwa na manufaa katika kukuza uchumi wakati ambao mikopo inapopungua kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa na pia wakati huu ambao soko la hati fungani la Ulaya limepungua kwa kiasi kikubwa.

Mkutano huo umezishirikisha nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo wenyeji Tanzania, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Sudani Kusini na Ethiopia.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter