Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tutahakikisha tunaondoa umaskini kwenye jamii: Serikali

Tutahakikisha tunaondoa umaskini kwenye jamii: Serikali

0 comment 93 views

Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha Tanzania inatimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 (SDGs).

Malengo hayo, ambayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kuondoa umasikini katika jamii.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Jenifa Omolo, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Natu El-maamry Mwamba amesema hayo wakati akifungua warsha ya wadau kwa ajili ya kuthibitisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa malengo ya Maendeleo Endelevu 2030, kabla ya kuwasilishwa katika Jukwaa la Juu la Siasa la Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani Mwezi Julai, 2023.

Serikali imewasilisha taarifa ya mapitio ya hiari ya nchi ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu 2030 kwa wadau kuijadili na kuipitisha.

“Mchakato wa kufanya mapitio ya utekelezaji wa SDGs umekuwa shirikishi, na wa uwazi, ukishirikisha wadau wote muhimu nchini wakiwemo Serikali Kuu, sekta binafsi, asasi za kiraia, Bunge, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na utafiti, pamoja na taasisi za elimu ya juu” amebainisha Omolo.

Amesema Tanzania, ilichagua kutekeleza ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu kwa kuyaasili katika mipango na mikakati ya kitaifa na ya kisekta.

Ameeleza kuwa wakati mchakato wa kupitishwa kwa SDGs unafanyika, Tanzania ilikuwa inaandaa mpango wake wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 – kwa upande wa Tanzania Bara, na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini 2016-2020 au MKUZA III, kwa upande wa Zanzibar.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa kutoka Wizara hiyo Dkt. Mursali Milanzi, amesema malengo yaliyofanikiwa katika ajenda kwa kipindi cha miaka mitano yametokana na ushirikiano wa wadau katika upatikanaji na matumizi ya takwimu.

Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa, Septemba 2015, zilipitisha ajenda ya 2030 ya kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambayo, pamoja na mambo mengine, iliainisha Malengo 17 ya Maendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter