Na Mwandishi wetu
Kama hatua mojawapo ya kuondoa matumizi ya kuni mkoani Kilimanjaro, mradi wa majaribio wa matumizi ya gesi asilia katika vijiji na taasisi za umma unatarajia kutekelezwa muda mfupi ujao katika wilaya ya Rombo mkoani humo.
Mtaalamu na msimamizi wa mradi huo Rigamba Wantae amesema gesi hiyo ambayo inatokana na kinyesi cha wanyama ilifanyiwa majaribio kwanza katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mamtukuna kabla ya kusambazwa rasmi katika wilaya hiyo.
Wantae amesema mpaka hivi sasa wamefanikiwa kuzalisha Unit 8,200 za umeme kwa ajili ya matumizi ya kupikia na ameongeza kuwa hivi sasa nguvu nyingi zinaelekezwa kuwafikia wananchi pamoja na taasisi za umma ambazo zimekuwa zikitumia kuni nyingi katika shughuli za kila siku kama kupika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo Agness Hokororo amesema kupitia mradi huo wa gesi asilia uharibifu wa mazingira utapungua kwa kiasi kikubwa. Ameongeza kuwa uharibifu wa mazingira unaotokana na kushamiri kwa shughuli za ukataji miti umepelekea ukame hasa katika ukanda wa tambarare wilayani hapo. Amewasihi wananchi kuanza kutumia nishati hiyo ya gesi asilia akisema kuwa utasambazwa katika maeneo mengi zaidi kadri siku zinavyokwenda.