Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amewataka waajiri nchini kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyakazi hususan wenye ulemavu ili kuwa na uchumi shirikishi na shindani.
Ridhiwani amebainisha hayo Oktoba 19, 2024 wakati wa kilele cha Bonanza la Afya la Waajiri lililofanyika kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam likiwa na kauli mbiu isemayo Zuia Magonjwa yasiyo ambukiza: Ongeza Ufanisi Kazini.
“Natambua kazi nzuri inayofanywa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kama sehemu ya Baraza la Ushauri la Taifa kwa wenye Ulemavu ambapo kupitia Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka imekuwa ikikitoa Tuzo Maalumu kwa Waajiri wanaojali ujumuishwaji wa wenye ulemavu mahali pa kazi” amesema.
Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na waajiri, Vyama vya Wafanyakazi na wadau wengine itaendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu, kiuchumi, kijamii, kisiasa sanjari na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2004, ili kutoa mwelekeo na mwongozo katika utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.
Aidha, Waziri Ridhiwani amesema Ofisi yake inaendelea na mchakato wa kufanya utafiti wa kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi, hivyo wadau waendelee kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni ili kufanikisha jambo hilo.
Awali akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa ATE Suzanne Doran, amesema Kauli mbiu ya Bonanza hilo inalenga kuongeza uelewa kuhusu
umuhimu wa kuzingatia masuala ya Afya na Usalama katika maeneo ya kazi na kuleta mjadala kuhusu umuhimu wa kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ili kuongeza ufanisi mahali pa kazi.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani kwa Nchi za Afrika Mashariki Caroline Mugalla, ametoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi kutambua na kukuza afya na ustawi wa wafanyakazi ili kupunguza athari mbaya za msongo wa Mawazo na mfadhaiko unohusiana na kazi.