Taasisi ya Uhasibu (TIA), imepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwaendeleza wanafunzi wenye mawazo ya kibunifu ili waweze kufikia malengo yao na kutekeleza Mpango wa Vituo Atamizi, unaowawezesha wanafunzi kujiajiri, kuajirika, na kuchangia uchumi wa Taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Jenifa Christian Omolo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kwenye sherehe za Mahafali ya 22 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika Kampasi ya Dar es Salaam Viwanja vya Kurasini ambayo ni Makao Makuu ya Taasisi hiyo.
Omolo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu ili kukidhi ongezeko la udahili.
“TIA ni miongoni mwa Taasisi zilizowezeshwa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 58.1, kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususan ujenzi wa miundombinu ya kusomea na kufundishia”,alisema Omolo.
Aliwapongeza uongozi na watumishi wa TIA kwa kusimamia vizuri rasilimali fedha na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na kwa umakini.
Aidha, Omolo aliwasisitiza Menejimenti ya Chuo kuhakikisha inaweka mipango madhubuti ili kuhakikisha miundombinu iliyopo kwenye Taasisi hiyo inatunzwa ili iweze kukaa muda mrefu na kutumika na watu wengi.
Akizungumza na Wahitimu Omolo aliwasisitiza kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya kwa lengo la kujifunza, kujitangaza kibiashara, na kujipatia kipato kwa kuwa ni rasilimali yenye nguvu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu, Prof. Jehovaness Aikael, aliwaasa wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho kwa kuonesha uadilifu na ufanisi.
“Mafunzo mliyoyapata hapa yakawe chachu katika jamii zetu kwa kuwa sisi ni wataalamu hivyo mkaipeperushe bendera ya TIA kwa kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mbalimbali na sehemu za kazi ili kuleta mabadiliko katika jamii,” alisema Prof. Aikael